Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda amewataka Walimu, Wazazi na Walezi kuhakikisha Wanafunzi wote walioandikishwa kujiunga na shule wnahudhuria masomo kwa wakati pasipo visingizio.
Kaganda ametoa wito huo, mara baada ya kutembelea shule mbalimbali za Msingi na Sekondari katika Wilaya hiyo, katika siku ya ufunguzi wa mwaka wa masomo 2025 huku akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kunakuwepo na mazingira bora ya elimu kwa wanafunzi wote.
Akizungumza na baadhi ya Wanafunzi, pia Mkuu huyo wa Wilaya aliwasihi kusoma kwa bidii, kuwaheshimu Walimu na kudumisha nidhamu, huku akiwataka Walimu nao kuendelea kusimamia malezi bora ya Kiafrika, ili kulinda na kuendeleza utamaduni wa Taifa.
Kwa upande wao Wanafunzi walimshukuru Kaganda na kuwasilisha salamu za shukrani kwa Serikali kwa jitihada za kuboresha elimu huku wakiahidi kusoma kwa bidii na kufikia malengo yao kitaaluma.
Ziara hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa watoto wote na kuhamasisha ushirikiano wa jamii katika kukuza elimu.