Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watuhumiwa watatu Kuva Zengo (25), Lukeresha Mlawa (32) na Bulanda Mathias (25)  kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili, Iddi Wilbroad Mjengwa (38) mkazi wa Igurusi na Maige Jifaru (44) mkazi wa Isunura na kuwajeruhi watu wengine watano huko Wilaya ya Mbarali.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga imeeleza kuwa Januari 10, 2025 katika Kitongoji cha Shitanda, Kijiji na Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo Wilaya ya Mbarali, ulitokea ugomvi baina ya familia mbili ya Mzee Rafael Ramadhani Mjengwa.

Mzee huyo ni mwenye hati namba MBLJ420 iliyotolewa mwaka 1987 dhidi ya familia ya Mzee Malewa, iliyosababishwa na mgogoro wa ardhi wa shamba lenye ukubwa wa ekari 1050, ambapo familia ya Mzee Malewa pia wanadai shamba hilo ni la familia yao, kwani wamekuwa wakilitumia kwa kilimo na kulisha mifugo kwa muda mrefu.

“Familia ya Mzee Rafael Ramadhani wakiwa wanaendelea na maandalizi ya kilimo katika shamba hilo, ghafla walishambuliwa na kundi la watu wapatao 15 wanaodaiwa kuwa ni wa Mzee Malewa na kusababisha watu wawili kufariki dunia na wengine watano kujeruhiwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na tukio hilo ufuatiliaji ulifanyika ambapo Januari 13, 2025 katika Kijiji na Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa kuhusiana na tukio hilo.

Wajengewa uwezo kufufua zao la Korosho Pwani
Lema amkataa Mbowe, ataka apumzike amuachie Lissu