Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Khatibu Kazungu amemueleza Balozi wa Tanzania huko Abu Dhabi, Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed umuhimu wa Tanzania kupata fedha za kutosha kutoka kwa wawekezaji, ili iweze kutekeleza miradi ya nishati jadidifu ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Dkt. Kazungu anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu katika Wizara hiyo, ambaye aliambatana na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Baraza la 15 la Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu IRENA, aliyaeleza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub alipokwenda kwenye ofisi za ubalozi huo kumtembelea.
Awali akizungumza kwenye kikao hicho Balozi wa Tanzania Abu dhabi, Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed alisema, Watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa za ajira zilizopo mjini Abu Dhabi kama ilivyo kwa nchi nyingine kama India, Kenya na Uganda ili kuinua uchumi wa nchi na kukuza kipato kwa wananchi wake.
Aidha, aliipongeza Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha umeme unakuwepo wa kutosha na wa uhakika hususani kwenye mradi wa treni ya mwendo kasi ambayo umekuwa na tija kwa wananchi na Serikali kwa ujumla
‘’Nitoe rai kwa Watanzania kuwa mabalozi wazuri wa mradi huu wa treni ya SGR pamoja na wataalamu wa TRC na TANESCO kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha hakuna hitilafu yoyote na watanzania wafurahie matunda ya mradi huo kutoka kwenye Serikali yao,” alisema.