Watu sita wamehukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji ya watu watatu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Dkt. Deo Nangela amesema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Januari 2, 2021 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, baada ya kuwaua kwa makusudi watu hao watatu ambao ni Muhozya Mchulo (32), Ndifin Luhamba (28) na Lunende Nyerere (29).
Waliohukumiwa ni Kija Jilunga (35), Salumu Ngelale (41), Singu Jilunga (31), Lutenganya Maduka (54), Ngwama Kulwa (37) na Musa Lufwega (49) ambao inadaiwa siku ya tukio waliwachoma na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuwatupa ndani ya mto kavuu, uliopo Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.
Jaji Nangela amesema, washitakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na kueleza adhabu hiyo imetolewa, ili iwe fundisho kwa washitakiwa na jamii katika kukomesha vitendo vya kikatili.

Makosa udhalilishaji wa Kijinsia yamepungua – DCI Chembera
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 17, 2025