Shirika la kutetea haki za Waandishi wa Habari – CPJ, limesema takriban wanahabari 67 wamefungwa jela barani kote Afrika, hali ambayo inaashiria changamoto inayoendelea kukwamisha uwepo wa Vyombo vya Habari huru.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mapema Januari 16, 2025 inaonesha kuwa kesi hizo kwa barani Afrika zinachangia jumla ya wanahabari 361, waliofungwa jela Duniani hadi kufikia Desemba 1, 2024 idadi ambayo ni ya pili kiukubwa kuwahi kurekodiwa na CPJ.
Mratibu wa programu ya CPJ barani Afrika, Muthoki Mumo amesema ripoti hiyo inaangazia mwelekeo wa Kimataifa ambapo tawala za kimabavu hutumia sheria kama zana za kukandamiza Wanahabari kwa kutumia sheria za usalama wa Taifa, kupambana na ugaidi na uhalifu wa mtandaoni, ili kuhalalisha ukandamizaji.
Amezitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Burundi, Ethiopia na Nigeria akisema zote zinatumia sheria iliyowekwa kwa ajili ya usalama wa umma, kufanya uandishi wa Habari kuwa kosa la jinai.
“Nchini Nigeria, kuna wanahabari wanne gerezani waliofunguliwa mashtaka chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni kuhusiana na ripoti zao kuhusu ufisadi na nchini Ethiopi Waandishi sita wapo gerezani. Watano kati yao wanakabiliwa na mashtaka chini ya sheria za kupambana na ugaidi. Wanaweza kukabiliwa na adhabu kali ikiwa watakutwa na hatia,” alifafanua zaidiMumo.
Aidha ameongeza kuwa, kwa Nchini Burundi Mwandishi wa chombo cha Habari za Mtandaoni ch La Nova, Sandra Muhoza alihukumiwa chini ya sheria za usalama wa Taifa baada ya kutuma ujumbe wa WhatsApp, kesi ambayo anadai ni mfano dhahiri kuwa uandishi wa Habari unachukuliwa kama kosa la jinai.