Wazazi na Walezi ambao wana Watoto waliojiunga na masomo katika shule mbalimbali Mkoani Simiyu, wametakiwa kuchangia chakula Shuleni, ili waweze kupata mlo akiwa masomoni kwa mujibu wa waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016.

Waraka huo ni ule wa kifungu namba 3.10 (iii) kinachoeleza wazi wajibu wa mzazi kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa na bweni kulingana na mazingira yao.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Khalifa Shemahonge amesema bado mwamko wa wazazi katika kuchangia chakula kwa Watoto wao uko chini, licha ya Wananchi wa Mkoa huu kujikita katika kilimo.

Amesema, “ukiangalia katika wanafunzi 654,000 wa shule za msingi mkoa mzima ni sailimia 56 pekee ndiyo wanaopata chakula kwa mwaka hivyo asilimia 44 watoto hawapati chakula wakati jamii ingekubali kujitoa tungekuwa na akiba ya chakula cha Watoto kwa mwaka mzima kwa sababu shughuli zetu kubwa ni kilimo na ufugaji.”

Awali mkazi wa Bariadi, Elizabeth Philemon alisema kiburi na mazoea baina ya wazazi yanarudisha nyuma jitihada hizo, huku akisema baadhi yao hufikiri kwamba anapochangia chakula shuleni anayefaidika ni mwalimu.

“Wewe mzazi huwezi kukaa kuanzia asubuhi hadi saa nane mchana bila kula vipi kuhusu mtoto anaweza kuvumilia? Wazazi wengine ni viburi tu si kwamba hawana michango wanafikiri kwamba tukitoa watakula walimu kumbe tunawatesa Watoto wetu,” alisema Elizabeth.

Kwa upande wake Mzazi Simon Kilulu ambaye ni fundi cherehani mjini Bariadi, amesema ugumu wa maisha bado unazikabili familia nyingi, kwani wapo baadhi wanashindwa kumudu mlo wa siku kwa familia na hivyo kutoweza kuchangia shuleni.

“Hali ni ngumu chakula kupata kwa siku ni shida Watoto utawalisha nini ,tunashinda na njaa siku zingine sasa unaweza kupata chakula cha kupeleka shuleni ,bado tuna hali ngumu sana sisi wazazi,” alisema Kilulu.

Hata hivyo, Shemahonge amewahimiza wazazi kutilia mkazo suala elimu ya awali, ili kila Mwanafunzi aliyeandikishwa darasa la kwanza afike akiwa tayari anajua KKK yaani Kusoma, Kuhesabu na Kuandika, ili kumrahisishia kazi mwalimu wa darasa la kwanza na kupunguza Watoto watakao feli darasa la nne.

Amesema, “mtoto aliyesoma elimu ya awali hawezi kuwa sawa na mtoto ambaye hajasoma awali tunampa kazi ya ziada mwalimu wa darasa la kwanza ambaye anawanafunza zaidi ya mia moja darasani amuangalie huyu ambaye hakupita awali hapo tutakuwa tunaongeza tu Watoto watakaofeli darasa la nne.”

Licha ya Serikali kufanya ukarabati, kujenga miundombinu na kutilia mkazo suala la elimu bila malipo, bado ugumu wa maisha unatajwa kuwa kikwazo kwa Wananchi kushindwa kuendeleza jitihada kwa kutoa michango Shuleni.

Haijawahi kutokea Halaand akiweka rekodi mpya Duniani