Mchezo wa Kariakoo Dabi ambao Yanga itaikaribisha Simba umepangwa kuchezwa Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hiyo inafuatia marekebisho ya ratiba ya ligi ambayo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeyafanya na kuyaweka hadharani jana.

Ratiba ya awali kabla haijafanyiwa marekebisho, ilikuwa inaonyesha kuwa miamba hiyo miwili nchini ingerudiana Machi Mosi mwaka huu baada ya mchezo wa duru la kwanza Yanga kushinda 1-0.

Ratiba hiyo mpya ambayo imetolewa jana, imeonyesha ligi itamalizika Mei 25 kwa uwepo wa mechi nane zitakazochezwa katika viwanja na miji tofauti.

Marekebisho hayo ya ratiba ya ligi yamefanyika baada ya kusogezwa mbele kwa fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) 2024 zilizopangwa kufanyika Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi hadi Februari 28 mwaka huu. Sasa zitafanyika Agosti 2025.

Kabla ya kuahirishwa kwa fainali za Chan, Bodi ya Ligi ilipanga kusimamisha Ligi Kuu hadi mwezi Machi mwaka huu.

Ratiba mpya iliyotoka inaonyesha kuwa Ligi itarejea kwa kuchezwa mechi mbili za viporo ambapo Februari Mosi Yanga itaikaribisha Kagera Sugar, wakati Februari 2 Simba itasafiri kwenda kuvaana na Tabora.

Baada ya hapo, mechi za raundi ya 17 zitaanza kuchezwa Februari 5 ambapo kutakuwa na mechi mbili pia ambapo Yanga itacheza na KenGold, Tabora itavaana na Namungo huku Simba ikirejea uwanjani Februari 6 kuvaana na Fountain Gate, huku Azam ikicheza na KMC.

Februari ligi itakapoendelea itakuwa ya kibabe kutokana na raundi sita kuchezwa ndani ya mwezi mmoja, kisha Machi ni raundi moja pekee ikifuatiwa na Aprili na Mei ambapo kila mwezi hapo zitapigwa raundi tatu kuhitimisha msimu huu ambao Yanga ni mabingwa watetezi wa taji la ligi hiyo.

Kwa sasa Simba inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 40, ikifuatiwa na Yanga (39), Azam 36 na Singida Black Stars (33).

Kule chini, KenGold inaburuza mkia ikiwa na pointi sita, juu yake kuna Kagera Sugar (11), Pamba Jiji (12) na Tanzania Prisons (14).

MECHI ZIJAZO

Februari 1, 2025

Yanga v Kagera Sugar (Saa 10:00 Jioni)

Februari 2, 2025

Tabora United v Simba (Saa 10:00 Jioni)

Februari 5, 2025

Tabora United v Namungo (Saa 8:00 Mchana)

Yanga v KenGold (Saa 10:15 Jioni)

Dodoma Jiji v Pamba Jiji (Saa 1:00 Usiku)

Februari 6, 2025

Tanzania Prisons v Mashujaa (Saa 8:00 Mchana)

Fountain Gate v Simba (Saa 10:15 Jioni)

Azam v KMC (Saa 1:00 Usiku)

Februari 7, 2025

Coastal Union v JKT Tanzania (Saa 10:00 Jioni)

Singida BS v Kagera Sugar (Saa 10:00 Jioni)

Ramovic afunguka kwa mara ya kwanza baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa
Maboresho huduma za afya: Tanzania imepiga hatua - Rais Samia