Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imepokea mwaliko kutoka Shirika la
Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), kwa ajili ya wafanyabiashara wa Tanzania kuwania Tuzo
za WIPO kwa Mwaka 2024.
Taarifa iliyotolewa hii leo Januari 22, 2024 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha BRELA imeeleza kuwa muda wa kutuma maombi ni kuanzia Januari 15 hadi Machi 31, 2025.
“Tuzo za WIPO zinatolewa kimataifa, na zinalenga kutambua na kusherehekea mchango
wa wajasiriamali wadogo na wakati, (SMEs) katika kutumia Miliki Ubunifu katika
uendeshaji wa biashara, na kuleta mabadiliko chanya kiuchumi, na kijamii kwa ujumla,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
BRELA imewahamasisha wajasiriamali wadogo na wa kati kuchangamkia fursa hiyo na
kushiriki katika kinyang’anyiro cha 2025 WIPO Global Awards katika sekta zote za
uchumi ikiwemo nyanja ya kiteknolojia, kilimo, viwanda vya ubunifu au nyanja nyingine.
Ili kupata tuzo hizo, BRELA inawaarifu wahusika kutuma maombi kwa lugha ya Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kirusi au Kijapani ambapo jopo huru la waamuzi litachagua hadi washindi saba watakaoalikwa kuhudhuria hafla ya Tuzo wakati wa Mkutano Mkuu wa WIPO utakaofanyika Julai, 2025 Geneva Uswizi.