Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imesema kuwa itaendelea na utoaji wa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini ili kuwawezesha wananchi katika maeneo ya vijijini kuwa na uelewa wa elimu ya fedha pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya fedha na kuweka akiba.

Hayo yamebainishwa na Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, wakati Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, iliyoambatana na Maafisa kutoka taasisi na wadau mbalimbali ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wakulima, waendesha bodaboda na wafugaji wa Tarafa ya Endabash, Wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha.

Kibakaya alieleza kuwa mfumo wa filamu unaotumiwa kutoa elimu ya fedha umewavutia wananchi kwa kuwa umekuwa mfumo rahisi utakaowawezesha kukumbuka kwa urahisi mafunzo waliyopata ya elimu ya fedha.

‘‘Kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kuhudhuria mafunzo ya elimu ya fedha inayotolewa kwa njia ya filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo uwekaji akiba, bima, utunzaji wa fedha na mada ya masuala ya uwekezaji wa masuala ya kifedha,’’ alieleza Kibaya.

Alisema kuwa Serikali iliona kuwa ni muhimu kuwapatia wananchi elimu ya fedha ili kuwawezesha kuwa na uelewa wa elimu ya fedha ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ikiwemo kutumia vema mikopo inayotolewa na Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Kibakaya alifafanua kuwa elimu hiyo ya fedha italeta mabadiliko kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa njia ya uwasilishaji kwa filamu itabaki kuwa kumbukumbu ya muda mrefu hivyo kuendelea kujenga mabadiliko ya usimamizi wa fedha binafsi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Endabash, Boisa Mandoo, aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata elimu ya fedha katika maeneo yao ambayo itawasaidia katika kusimamia matumizi ya fedha pamoja na kutumia huduma za fedha zinazotolewa na watoa huduma waliosajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Program ya kutoa elimu kwa Umma ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 ambapo unalenga kufikia wananchi asimia 80 hadi kufikia mwaka 2025/26 pamoja na utekelezaji wa Programu ya Elimu ya Fedha kwa Umma ya mwaka 2020/21 – 2025/26.

Sheria mpya: Watoto wa miaka 9 ruksa kuolewa Nchini Iraq
Zero zapungua Matokeo kidato cha nne - Dkt. Mohamed