Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuboresha ushirikiano na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kuondoa urasimu wa kuwazungusha Wananchi wakati wanapokuwa katika mchakato wa kutafuta Kitambulisho cha Taifa.
Bashungwa ameelekeza hayo leo tarehe 23 Januari 2025 wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya dara ya Uhamiaji, Dodoma ambapo ameitaka Idara hiyo kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa Wananchi.
Bashungwa amemtaka Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji CGI, Dkt. Anna Makakala kuhakikisha kila Ofisi ya Wilaya ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inakuwa na Afisa wa Uhamiaji ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi.
“Nitakapokuwa naenda kwenye Wilaya, nikifika ofisi za NIDA nikute kuna Afisa wa NIDA lakini awepo Afisa wa Uhamiaji ambao wanashirikiana kuwahudumia Wanzania ili kuepuka upumbufu kwa Wananchi na Malalamiko yasiyokuwa na tija ” amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuendelea na Operesheni, misako na doria za kukamata wahamiaji haramu na kuhakikisha wageni wote wanaoingia ndani ya nchi, wanafuata tararibu na sheria za kuingia nchini.
Kadhalika, Bashungwa ametoa onyo kwa baadhi ya Maafisa wa Idara ya Uhamiaji ambao sio waaminifu, wanaowaonea Wananchi wakati wa Operesheni na misako inapofanyika.
Awali, Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji CGI, Dkt. Anna Makakala ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji inaendelea na misako, doria na kaguzi mbalimbali kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa.
“Katika mwaka 2024 tumefanya Oparesheni, mikasako na doria nchi nzima, jumla ya Wahamiaji wa makosa mbalimbali 14,368 walikamatwa na kuchukuliwa hatua ” ameeleza CGI, Dkt. Makakala.
“Nimeelekeza Idara ya Uhamiaji na NIDA kushirikiana ngazi za wilaya maafisa wote wa NIDA na Uhamiaji wawepo ofisi moja wakati wanahudumia wananchi ili kuondoa usumbufu wa wananchi kutoka ofisi moja kwenda nyingine na wakati taasisi zote 2 zipo ndani ya Wizara moja na wilaya moja.
Nitakapokuwa napita huko kwenye wilaya tutasimamia ipasavyo utekelezaji wa hili jambo kupitia mrejesho wa wananchi,” alisema.