Vijana wametakiwa kuendelea kuenzi utamaduni za kitanzania na kutosahau asili ya walipotoka ili kuondosha malalamiko ya kuporomoka kwa maadili.
Naibu Makamu Mkuu wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, Prof. Razack Lokina ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya mwaka mpya wa Kichina unaojulikana kama mwaka wa Nyoka, ikiwa ni sehemu ya kudumisha utamaduni wao yaliyoandaliwa na taasisi ya conficius chuoni hapo.
Amesema, “huu ni utaratibu mzuri kwasababu unamfanya mtu popote alipo duniani kuweza kudumisha utamaduni wake na hapa tumeona bila kusahau tunaona kizazi cha sasa hivi kina tabia ya kujisahau lakini tumeona wenzetu wa kichina muda wote wanaendelea kudumisha utamaduni wao.”
Aidha, Prof. Lokina ameipongeza Serikali kwa kurudisha somo la historia shuleni ambalo litawakumbusha Wanafunzi walipotoka ili waweze kuendelea kuishi kwenye utamaduni wao licha ya kuwa kwasasa dunia ipo kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Lugha na Utamaduni wa Kichina Chuo Kikuu cha Dodoma – UDOM, Dkt. Rafiki Sebonde amesema mwaka mpya wa kichina husherehekewa kwa kufuata aina za wanyama na kwa mwaka huu kwao ni mwaka wa nyoka.