Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameshuhudia utiaji saini mikataba 9 yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 4.7 ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na wakandarasi.

Hafla hiyo imefanyika leo, Januari 24, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Chama.

Akizungumza katika hafla hiyo,RC  Macha ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha na kutekeleza miradi ya maji mkoani Shinyanga, akielezea kuwa juhudi hizo zitasaidia kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi.

Macha ameeleza kuwa mikataba hiyo ni ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 4.7, ambapo vijiji 16 vitapata huduma ya maji, na vituo 18 vya kuchotea maji vitajengwa.

Amesema kuwa, kupitia utekelezaji wa miradi hii, Mkoa wa Shinyanga utaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 68 hadi asilimia 70 ifikapo mwisho wa mwaka 2025.

Macha amewataka wakandarasi kutekeleza miradi hiyo kwa weledi na kumaliza kwa wakati, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wakandarasi kushirikiana na wananchi katika maeneo ya miradi, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwao.

RC Sendiga afungua kikao cha maboresho ya kodi
Wakurugenzi tatueni changamoto za Wakulima - Bashe