Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Remija Salvatory ameshiriki zoezi la kuwasilisha sare za shule kwa wanafunzi wa Shule za Msingi ambao wazazi wao hawajiwezi, na kupanda miti katika Shule ya Msingi Makulu jijini Dodoma, Siku ya Elimu Duniani, Januari 24, 2025.

Tukio hilo lililoratibiwa na C FM Radio kupitia Kampeni ya ‘Nipendezeshe Nisome’, limehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj. Jabir Shekimweri.

Zaidi ya sare za shule 400 zilizotolewa na wadau wa elimu ikiwa ni pamoja na PPRA, zimewasilishwa kwa wanafunzi walioanishwa na maafisa elimu kutoka Wilaya za mkoa wa Dodoma.

Remija amesema PPRA imechangia sare za shule kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora inayotolewa bure.

Aidha, amesema watoto hawa wanapopata elimu ndio watakaokuwa wataalam wa ununuzi na ugavi, wajenzi wa mifumo ya kielektroniki, wazabuni na wadau wa ununuzi wajao.

Remija ameongeza kuwa PPRA inahamasisha ununuzi wa umma endelevu (Sustainable Public Procurement), unaozingatia utunzaji wa mazingira pamoja na mambo mengine, hivyo, kupanda miti katika shule hiyo ya msingi ni kuendelea kulinda mazingira na kuwajengea watoto utamaduni wa kutunza mazingira hayo ili nayo yatutunze.

 

Faru Mweusi aitoa kimasomaso Tanzania
Maisha: Mtego rahisi wa kumnasa Mwanamke msaliti