Bondia wa timu ya Taifa ya ngumi, Faru weusi wa Ngorongoro, Lucas Mwajobaga amefanikiwa kiubuka na ushindi wa kibabe dhidi ya Liduema Elder kutoka Angola katika mapambano ya kwanza ya semi-pro ya usiku wa Solidarty & Fratenity Boxing Gala (Mshikamano na Udugu) katika uwanja wa ndani wa Ammar Dakhlaoui, Tunis, Tunisia.
Rais wa shirikisho la ngumi la Taifa BFT, Lukelo Wililo amethibitisha ushindi huo wa bondia huyo alioupata kwa kukusanya ‘points’ za majaji wote watatu dhidi ya Liduema Elder kutoka Angola.
Wililo amesema ushindi huo umemfanya Mwajobaga kuwa bingwa baada ya kubeba mkanda wa Afrika katika uzani wa Light welterweight yaani kilo 63.5.
“Tumefungua mwaka vizuri kwa kuliheshimisha Taifa letu Kimataifa, na ushindi huu wa mkanda wa Afrika wa mshikamano na udugu ni zawadi tosha kwa Amiri jeshi mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa askari wake Lucas,”amesema Willilo, ambae ameambatana na bondia nchini Tunisia.
King Lucas na Mwalimu wake Samwel Kapungu “Batman” wanatarajia kuanza safari ya kurejea nchini Tanzania leo jumamosi kwa usafiri wa shirika la ndege la Uturukii na kuwasili Dar es salaam siku ya jumapili ya januari 26, 2025 saa tisa usiku.