Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) imeweka hadharani ratiba ya Ligi Kuu Bara inaonyesha mwezi ujao ambao ligi hiyo itarejea baada ya kusimama kwa muda, utakuwa na mechi nyingi zaidi. Katika mwezi Februari pekee zitachezwa mechi 50 sawa na raundi sita vikiwemo viporo viwili.

Simba na Yanga zenye rekodi ya kubeba ubingwa wa ligi mara nyingi zaidi ya timu zote zina dakika 630 sawa na mechi saba kila moja kabla ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo. Mechi hizo zimekaa kimtego katika mbio za ubingwa.

Kwa ujumla timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo zitacheza si chini ya mechi sita Februari, jambo ambalo linatoa picha kwamba mwezi huo unaweza kuamua hatima ya timu nyingi katika kufikia malengo.

Kwa zile ambazo zinapambana zisishuke daraja, Februari ndio wakati mzuri wa kuchanga karata na hata zinazowania nafasi nne za juu ikiwemo ubingwa – muda ndio huo kwani zikiteleza hapo inaweza kuwa ndio zimetoka nje ya malengo.

Wakati ligi ikirejea, Simba inayoongoza msimamo itacheza dhidi ya Tabora United ugenini ilhali Yanga inayoshika nafasi ya pili itaikaribisha Kagera Sugar.

Timu hizo zimepishana pointi moja pale juu kwenye msimamo, hivyo hesabu zao ni kuona Februari inamalizika vizuri kabla ya mechi yao itakayopigwa Machi 8 ambayo huenda ndiyo ikaamua zaidi mbio za ubingwa kwa wakongwe hao.

Ukiwaweka kando mafahari hao wawili, Azam na Singida Black Stars nao hawapo mbali kwani zinashika nafasi ya tatu na ya nne. Tofauti ya Azam na kinara Simba ni pointi nne wakati Singida ikiachwa pointi saba.

YANGA

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara na washindi mara nyingi (30) wa taji hilo, wana nafasi ya kurejea kileleni kwani ligi ikirudi mechi yao dhidi ya Kagera Sugar ndiyo ya kwanza kuchezwa ikipangwa kupigwa Februari Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Kagera haipo vizuri kwenye msimamo, inashika nafasi ya pili kutoka chini ikikusanya pointi 11. Mchezo huu kwao wanautazamia zaidi kutokana na kwamba mzunguko wa kwanza nyumbani kufungwa 2-0 na Yanga.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha Kagera mbele ya Yanga imekuwa na matokeo mabaya zaidi. Tangu 2010/2011, timu hizo katika ligi zimekutana mara 29, Kagera imeshinda 4, huku Yanga ikishinda 23 na sare 2.

Yanga ikitoka hapo, Februari 5 itaikabili KenGold, timu ambayo ipo nafasi ya mwisho na pointi zake sita. Safari hii, Yanga inakwenda kukutana na timu ambayo imefanya maboresho makubwa ya kikosi chake kupitia usajili wa dirisha dogo ikishusha nyota wapya 23 wakiwemo wazoefu waliowahi kutamba Simba na Yanga kama Bernard Morrison, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani na Zawadi Mauya. Mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 ugenini.

Yanga itacheza mechi ya tatu Februari 10 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. JKT Tanzania imekuwa ngumu kufungika nyumbani msimu huu kwani haijapoteza mechi yoyote ikiwa hapo, imeshinda tatu na sare nne ikiwa na clean sheet tano katika mechi hizo saba. Kumbuka haijaruhusu mabao zaidi ya mawili, hivyo utakuwa mchezo mgumu kwa Yanga licha ya kwamba mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda nyumbani 2-0.

JKT Tanzania haina matokeo mazuri mbele ya Yanga, katika mechi tano za mwisho, imeambulia sare moja tu huku vichapo vinne.

Yanga itaendelea kuwepo Dar, safari hii itaikabili KMC, Februari 15 kwenye Uwanja wa KMC Complex. Mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda 1-0 wakati KMC ikinolewa na Kocha Abdihamid Moallin ambaye hivi sasa yupo katika benchi la ufundi la Yanga akiiacha KMC mikononi mwa Kally Ongala.

Bata la Dar kwa Yanga litaishia Februari 17 pale itakapoikaribisha Singida Black Stars. Timu hizo zilipokutana mzunguko wa kwanza mechi ikichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga ilishinda 1-0.

Singida Black Stars kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ina pointi 33, inapambana isitoke nje ya nafasi hizo, hivyo mechi zake hizi za mzunguko wa pili lazima zitakuwa na ushindani mkubwa hasa ikikutana na zile zilizo juu yake.

Februari 23 itakuwa Kigoma kucheza na Mashujaa. Mzunguko wa kwanza Yanga ilishinda 3-2 huku Prince Dube akitupia hat trick ya kwanza ya ligi msimu huu ambayo hadi sasa imebakia kuwa ni hiyo tu.

Ikitoka Kigoma itakwenda Mwanza kuikabili Pamba Jiji timu ambayo mzunguko wa kwanza ilifungwa na Yanga 4-0. Kumbuka Pamba Jiji nayo haipo sehemu salama sana kwenye msimamo, inashika nafasi ya 14 na pointi zake 12.

Yanga inaweza kuitumia vizuri fursa ya kucheza mechi tano mfululizo jijini Dar es Salaam katika kuweka sawa hesabu zake kabla ya kutoka kwenda Kigoma na Mwanza, kisha kukutana na Simba Machi 8.

SIMBA

Ipo kileleni na pointi 40. Wakati inamaliza mzunguko wa kwanza, kocha mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids alisema wamefanikisha malengo kwani alikuwa na hesabu za kukaa kileleni kisha mzunguko wa pili kuja na hesabu zingine za kuishikilia nafasi hiyo.

Katika kutimiza malengo ya mzunguko wa pili, Simba ina mechi saba za kukimbizana na Yanga kabla ya mchezo wao wa Kariakoo Dabi. Katika mechi hizo saba tatu itakuwa Dar na nne nje huku mechi moja ikiwa ni dhidi ya Azam, timu ambayo nayo haipo mbali kwenye msimamo ikikamata nafasi ya tatu na pointi 36. Tofauti yao ni pointi nne kwa sasa.

Februari 2 Simba itakuwa ugenini wakati ligi ikirejea kwenda kukabiliana na Tabora United, timu inayoonekana kuwa imara zaidi nyumbani na hata ugenini kwani mzunguko wa kwanza iliifunga Yanga 3-1.

Tabora United mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Simba ilipoteza kwa mabao 3-0, wakati huo iliwakosa baadhi ya wachezaji wake wa kimataifa waliokuwa hawajakamilisha usajili. Mechi nane za nyumbani msimu huu, Tabora imepoteza moja, sare tatu ikishinda nne dhidi ya Azam, Mashujaa, Pamba Jiji na Kagera Sugar.

Februari 6, ni mtihani mwingine wa Simba itakapokuwa ugenini kukabiliana na Fountain Gate, mzunguko wa kwanza ilishinda 4-0. Kwa sasa Fountain ina kocha mwingine, Robert Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya.

Baada ya mechi mbili za ugenini, Februari 11 Simba itakuwa nyumbani kukabiliana na Tanzania Prisons yenye kocha mpya, Aman Josiah.

Mzunguko wa kwanza Simba ilishinda 1-0 ugenini. Msimu uliopita Prisons iliifunga Simba 2-1 ugenini, hivyo ni timu ambayo inaweza kuwashangaza.

Simba itabaki tena Dar kucheza na Dodoma Jiji, itakuwa Februari 15, wakati mzunguko wa kwanza Simba ikishinda 1-0 huku mechi tisa walizokutana tangu 2020/2021, Simba imeshinda zote na saba za mwisho ikiondoka na clean sheet.

Februari 19, Simba itakwenda Ruangwa mkoani Lindi kucheza dhidi ya Namungo, wapinzani ambao wamekuwa wagumu sana kwao tangu waanze kukutana kwenye ligi 2019-2020.

Licha ya kwamba mzunguko wa kwanza Simba kushinda 3-0 nyumbani, lakini inapokwenda kwa Namungo inajiuliza maswali mengi kutokana na mechi tano ilizokwenda huko imeshinda moja pekee, nne zikiwa sare. Namungo ikiwa nyumbani ni mpinzani mgumu kwa Simba.

Funga kazi itakuwa Februari 24, Simba ikiikaribisha Azam baada ya mzunguko wa kwanza kushinda 2-0 ikiwa ugenini. Azam inapokutana na Simba, inakuwa mechi ngumu kutokana na timu hizo kila msimu kuwa ndani ya tatu bora zikiwania ubingwa na kushiriki kimataifa. Ikitoka kucheza na Azam, kabla ya kukutana na Yanga, Simba itakwenda ugenini kukabiliana na Coastal Union, Machi 1.

Coastal Union chini ya Juma Mwambusi, itaikaribisha Simba baada ya mzunguko wa kwanza matokeo kuwa 2-2. Sare ambayo Simba iliongoza 2-0 hadi mapumziko, Coastal ikachomoa mabao yote kipindi cha pili.

Kuhusu mbio hizo za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema: “Baada ya kufuzu robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika, tunaendelea kupambana kwa ajili ya mafanikio katika mashindano ya ndani pia. Tunaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi moja mbele ya Yanga, pia tuna mchezo wa Kombe la FA, wikiendi ijayo. Haya yote ni mashindano makubwa ambayo lazima tuyazingatie.”

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amebainisha kuwa kilichobaki kwao hivi sasa ni kutetea ubingwa wa ligi baada ya kuishia makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ulega ataka tathmini ya TEMESA ujenzi wa Vivuko vipya
Faru Mweusi aitoa kimasomaso Tanzania