MSHAMBULIAJI mpya wa Juventus, Randal Kolo Muani anatazamiwa kucheza mechi yake ya kwanza Jumamosi kwenye Serie A huko Napoli, kocha mkuu Thiago Motta alifichua Ijumaa.
Juve ilimsajili fowadi wa Ufaransa Kolo Muani kutoka Paris Saint-Germain kwa mkopo siku ya Alhamisi, na kuwa usajili wao wa pili katika dirisha la uhamisho la Januari baada ya kuwasili kwa beki wa kulia Alberto Costa.
“Randal anapatikana na tutaona kama anaanza au la. Ni muhimu kumchukua mchezaji wa kiwango chake kwa sababu tunadhani anaweza kuisaidia timu kushinda michezo,” Motta aliwaambia waandishi wa habari.
Kuimarishwa kwa Juve kumekuja kwa wakati mwafaka, huku mabeki Bremer na Juan Cabal wakiuguza majeraha ya kano za mbele na mshambuliaji Arkadiusz Milik pia hayupo kwa muda mrefu.
“Muungano wa waliowasili unaendelea vizuri sana. Kesho kila mtu atakuwepo isipokuwa Bremer, Cabal na Milik,” Motta alisema.
Wakati huo huo, Dusan Vlahovic huenda akawa kwenye benchi kwa mara ya tatu mfululizo Jumamosi baada ya Motta kusema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anapambana na masuala ya utimamu wa mwili.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Serbia pia amekuwa akihusishwa na uhamisho mwezi huu, huku Chelsea na Arsenal zikitajwa kuwa huenda zikatua.
“Randal na Nico (Gonzalez) wanaweza kucheza winga. Dusan alicheza sana na alikuwa na tatizo la kimwili. Tutaona kesho nani ataanza na nani ataingia kwenye mechi,” Motta aliongeza.
Bianconeri ndio timu pekee ambayo haijafungwa kwenye Serie A, lakini sare 13 katika michezo 21 imewafanya wabaki nafasi ya tano kwenye msimamo na pointi 13 nyuma ya vinara Napoli.
Motta alisema Partenopei wa Antonio Conte “anastahili katika nafasi ya kwanza”, lakini akaongeza kuwa wachezaji wake wako katika hali ya kujiamini baada ya kushinda AC Milan mara ya mwisho.
“Nimeridhishwa na mambo mengi na mengine kidogo, kama vile sare nyingi, lakini tayari nimelizungumza. Wazo letu ni kufanya kazi kubwa wakati wa wiki ili kupata ushindi,” Motta alisema.
“Kumekuwa na mabadiliko mengi kwenye kikosi, mabadiliko ni muhimu kwa sababu tofauti. Kesho tutacheza mechi kubwa ambayo ni Napoli dhidi ya Juventus.”