Swaum Katambo – Katavi.

Wananchi mkoani Katavi wametakiwa kutoficha matatizo yanayohitaji msaada wa kisheria na badala yake kutumia fursa ya uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, maarufu kama Samia Legal Aid  Campaign.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati akizindua Kampeni hiyo katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashaulili vilivyopo mjini Mpanda ametia wito huo na kuwataka Watendaji watakao wahudumia Wananchi kutowatoza fedha, kwani zoezi hilo ni bure.

Amewataka wazazi na walezi wa watoto waliofanyiwa ukatili kushirikiana na wataalamu wa sheria ili haki iweze kutendeka huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuimarisha huduma za kisheria hasa kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia, watoto, na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.

Alisema matarajio yake ni kuona migogoro mbalimbali ya kisheria kama ya ardhi, ndoa, mirathi, migogoro inayohusiana na ukatili wa kijinsia, migogoro ya kukosa matunzo kwenye familia itakwenda kupungua mkoani humo kwa kiasi kikubwa.

Awali akitoa maelezo ya Kampeni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin J. Rwezimula alisema lengo kuu la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa watu wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.

Alieleza kuwa kampeni hiyo itahusisha utoaji wa elimu kuhusu haki zinazohusu ardhi, ndoa, mirathi, madai, jinai, na haki za binadamu kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kupitia kampeni hiyo, Serikali inalenga kupunguza migogoro ya kisheria na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya sheria kwa njia ya mafunzo na huduma za moja kwa moja.

Aidha Dkt.Rwezimula ameiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili waweze kuwafikia wananchi kwa wakati.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Boniface Butondo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kuwa misaada hiyo ya kisheria itakwenda kuwasaidia hasa katika sheria kandamizi alizozitaja kuwa ni sheria dume katika masuala ya mirathi, mashamba pamoja na migogoro ya ardhi.

Butondo alieleza kuwa pamoja na mafanikio yanayopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wananchi bado wanapaswa kufahamu haki zao za msingi ili waweze kujilinda na kuchangia katika maendeleo ya nchi akisema elimu ya kisheria ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, umeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, huku wengi wakisifu jitihada za Serikali za kupeleka huduma za msaada wa kisheria hadi ngazi za mikoa, Kampeni hiyo inatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kupunguza ukatili, migogoro ya kijamii, na kuimarisha utawala wa sheria nchini.

Mwisho.

EPL:Ni Chelsea au Liverpool kuingia TOP FOUR leo
Michel awataka Girona kulipa kisasi baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa