Ligi kuu Uingereza inaendelea wikiendi ya leo kwa mchezo muhimu na mgumu unaowakutanisha Chelsea wakiwa Ugenini dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City. Mchezo huu utatoa taswira nani ataingia au kusalia nafasi 4 za juu katika raundi ya 23. Chelsea wana alama 40 kwenye mechi 22 wakishika nafasi ya 4 na Manchester City wana alama 38 wakishika nafasi ya 5 baada ya mechi 22.
Tathmini ya Mchezo
Chelsea na Manchester City zote zinawania ubingwa wa EPL ambao kwa sasa unapewa nafasi kutwaliwa na Liverpool wenye alama 50 pointi 10 zaidi ya Chelsea na 12 dhidi ya Manchester City. Kama mchezo utamalizika na Chelsea kushinda mchezo basi watakuwa na alama 43 wakisalia nafasi ya 4 wakisalia nyuma ya Arsenal na Nottingham Forest wenye alama 44.
Kama City wataibuka na ushindi katika mchezo huo watafikisha alama 41 na kuwashusha chini Chelsea na watakuwa na utofauti wa alama 3 dhidi ya Arsenal na Nottingham Forest.
Historia yao kwa misimu ya Karibuni
Manchester City na Chelsea wamecheza jumla ya mechi 57 za mashindano mbalimbali .Manchester City ameibuka na ushindi wa michezo 27 wakifunga mabao 75 wakati chelsea ameibuka na ushindi wa michezo 23 akifunga mabao 67. Timu hizi zimetoka sare mara 7. na mchezo wa leo ni mchezo wa 58. Kwa michezo mitano iliyopita Manchester City amekuwa kinara akishinda mara 5 kwenye mashindano mbalimbali.
Guardiola kurejesha matumaini ya mbio za ubingwa
Msimu wa 2024/25 ni moja ya changamoto ambayo Guardiola amekutana nayo tangu awe kocha. Ushindi wa mechi 11 kati ya 22 akiruhusu kufungwa mechi 6 na sare 5 ni vitu vinavyompa mtihani mkufunzi huyo.City ya sasa ni kama haijatengemaa baada ya kuruhusu kufungwa mabao 29 sawa na wastani wa kuruhusu bao moja na robo kwa kila mechi anayocheza. Kupoteza mchezo wa leo kutazidi kuzima matazamio ya klabu kuelekea ubingwa.
Usajili wa beki wa kati Vitor Reis,Abdukodir Khusanov naOmar Marmoush kunaweza kurudisha kiwango cha CITY ambao wanaonekana kupoteana.
Marlesca kurudisha makali ya Chelsea
Mashabiki wa Chelsea wameanza kukosa mwelekeo baada ya kushinda mchezo mmoja tu kati ya 6 ya EPL waliyocheza hivi karibuni. Chelsea walipoteza mchezo dhidi ya Fulham na Ipswich mwezi Disemba 2024 kisha sare mchezo wa Crystal Palce na Bournemouth na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves. Matokeo dhidi ya City yanaweza kurejesha au kudidimiza mipango ya klabu hiyo kwa msimu huu.