Boniface Gideon – Tanga.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imesema itatumia siku ya wapendanao (Valentine Day) kwa ajili ya kuyatangaza mapango ya Amboni kupitia Programu ya Diko la Amboni ambayo itahusisha mashindano ya kupika vyakula vya asili ikiwa ni sehemu ya kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha amewataka wakazi wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi na kusherehekea siku hiyo kwenye mapango ya Amboni ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utalii wa ndani lakini pia amewataka wananchi kuhakikisha siku ya Valentine hawatafuti sehemu ya kwenda bali wafike katika mapango hayo.

Kubecha ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Tanga uliofanyika kwenye mapango hayo na kuhusihusisha vikundi mbalimbali vya ngoma za asili.

Akizungumza kwenye mkutano huo Kubecha amewataka wananchi kutumia vizuri uwepo wa siku hiyo kutangaza vitu vingine vya asili ikiwemo vyakula.

“Amboni sehemu tulivu, rafiki, na ni sehemu nzuri ya kustawisha huba la mapenzi niwaombe wananchi wa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kuvuka mpaka na kuungana nao siku hiyo ya Diko la Amboni na kwamba hawatojuta kufika Amboni, “alisema Kubecha.

“Tumesikia hapa kutakuwa na mashindano ya wapishi katika siku hiyo lakini pia mavazi wale wenye mavazi ya asili wajitokeze kwakuwa nayo yatahusishwa siku hiyo kama ambavyo mimi hapa leo nimevaa msuli na kanzu vyote hivi ni kuonyesha kwamba jambo hili tunalithamini, “alisisitiza Kubecha.

“Kwakweli siku hiyo ambayo tutashindanishwa mimi nitaomba jiko ili niingie jikoni na mimi nionyeshe uhodari katika kuchangamsha utalii wa mapishiTanga ni mahodari kwenye enwo la mapishi hivyo siku hiyo nina imani wanatanga watajitokeza kuonyesha uhodari wao, “alisema Kubecha.

Kubecha amesema jambo hilo pia litaongeza utalii wa vipando kama baiskeli usafiri ambao zamani ulikuwa ndio pekee kwa jamii ya watu wa pwani ambapo ametaka siku hiyo watu wafike kwenye mapango hayo kwa kutumia usafiri wa baiskeli wakiamini maandalizi yaliyofanywa kuanzia leo hadi tarehe 14 ya mwezi wa pili ambayo ndio itakuwa siku ya kilele ya Diko la Amboni.

Kamishna msaidizi Mwandamizi kutoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro anayeshugjulikia huduma za utalii Mariam Kobelo amesema lengo la siku hiyo ni kuiweka jamii pamoja na kukitangaza kivutio cha Amboni wakiamini Tanga ndipo mapenzi yalipozaliwa na kwamba wapo sehemu sahihi kutumia siku ya wapendano kutangaza kivutio hicho.

Amesema shughuli hiyo ambayo itafanyika rasmi tarehe 14 mwezi februari mwaka huu wanaamini itakwenda kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia kwa Mkoa wa Tanga.

Mwigulu: Nishati ni muhimu kwa uchumi wa jamii
Asilimia 80 ya ajira huundwa na Biashara ndogo - Banga