Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, unatarajiwa kuanza Januari 28 hadi Februari 14, 2025 Jijini Dodoma ukiwa ni mahsusi kwa ajili ya Kamati za Kudumu za Bunge kuwasilisha Taarifa za Mwaka za Shughuli za Kamati kwa kipindi cha Januari 2024 hadi Januari 2025.
Taarifa iliyotolewa hii leo Januari 27, 2025 na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma cha Bunge imeeleza kuwa katika Mkutano huu, Bunge linatarajia kujadili na kupitisha Miswada mitano ya Sheria ambayo ilisomwa Mara ya Kwanza katika Mikutano iliyopita.
Miswada hiyo ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2024 [The written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.3) Bill 2024] na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2024 [The written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4) Bill
2024].
Mwingine ni Muswada wa Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania wa Mwaka 2024, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024 [The Environmental Management (Amendments) Bill, 2024] na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kazi wa Mwaka 2024. [The Labor Laws (Amendments) Bill, 2024].
Aidha, taarifa hiyo pia imeeleza kuwa wastani wa Maswali ya Kawaida 250 yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali na kutakuwa na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwa siku za Alhamisi.
Ratiba yote ya Mkutano wa Bunge inapatikana katika Tovuti ya Bunge ya www.bunge.go.tz.