Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Simon Mpandalume amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani humo ili kuwaletea maendeleo wananchi hasa ikizingatiwa makusanyo ya ndani ya halmashauri yamezidi yameongezeka.
Mpandalume ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyigogo (CCM), ametoa kauli hiyo jana tarehe 27 Januari 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Yichobela kwenye mkutano wake wa hadhara.
Katika mkutano huo pia ulihudhuriwa na madiwani wenza kutoka kata ya Bukandwe (Marco Minzi) na Kongoro (Herbet Faustine) pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM katika ngazi ya wilaya, kata na Kijiji.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano huo, Mpandalume alisema wakati anaingia madarakani 2020 halmashauri hiyo ilikuwa inakusanya Sh. bilioni 2.4 lakini sasa inakusanya Sh bilioni 5.2.
“Nikawaambia wenzangu hapana… fedha hii ni kidogo haitoshi kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi, Magu ni kubwa kwa sababu Mwanza nzima inajengwa na mchanga na mawe kutoka Magu, stendi zetu zinakusanya fedha nyingi mno.
“Nikawaambia madiwani wangu wote tuendeni ‘site’ tukakusanye fedha za wananchi wangu ambazo zinapotea… leo tunakusanya Sh bilioni 5.2 kwa mwaka,’ alisema.
Alisema fedha hizo sasa ndizo zinazokuja kwenye miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa shule za msingi na sekondari 32 pamoja na zahanati.
Aidha, alisema fedha hizo zimesaidia ujenzi wa stendi ya Ilungu ambayo sasa ujenzi wake unaelekea kwenye boma.
“Stendi kuja Ilungu tafsiri yake ni kwamba kuanzia Nyanshimba, Ichobela na Kinango maeneo haya yanaenda kupanda thamani, tayari kuna fedha ya Sh milioni 130 ya kujenga stendi yetu… tayari tumeanza na boma linaanza kunyanyuka wiki hii. Tutaenda kufanya kazi pale za biashara. Stendi ina faida kubwa kwenye kata hii,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa nyumba ya mganga wa zahanati ya Yichobela, alisema katika mwaka wa fedha wa 2025/2026 imetengewa bajeti kumalizia kukamilisha ujenzi wake.