Wakulima wa mazao ya biashara mkoani Simiyu, wameazimia kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kuuza mazao yao, ili kukabiliana na ulaghai unaofanywa na walanguzi wa mazao hayo wanaowasababishia hasara.
Maazimio hayo, yamefanyika katika kikao cha pamoja kilichojumuisha Wakulima na Wadau wa mazao chini ya usimamizi wa mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko, kilichoketi katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Simiyu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Irene Mlola amesema mfumo unaowekwa unamhusisha kila mkulima kwa kumpa nafasi ya kupendekeza maghala yatakayo hifadhiwa nafaka hizo, yatakayokuwa na Wafanyabiashara rasmi waliosajiliwa watakao nunua mazao hayo kwa pesa taslimu.
Amesema, “kila mklima atapata haki ya kuchagua maghala ambayo anataka mazao yao yahifadhiwe na sisi tutayakagua na kujiridhisha kisha tutayasimamia na wale wakulima wadogo kuna watu ambao tumewarasimishaili waweze kununua mazao kwao na kuyaleta ghalani kwa pesa taslimu.”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi amesema mfumo huo utatoa takwimu halisi za Wafanyabiashara wa mazao hayo, ili yule ambaye hatokuwa katika mfumo asiwe na haki ya kununua mazao kutoka kwa mkulima kwa lengo la kudhibiti mapato kwa Halmashauri.
Amesema, “kama mtu hajasajiliwa asije kununua ili na sisi tuwe na takwimu sahihi za idadi ya wafanyabiashara tulio wasajili ambao wananunua nafaka na kuchangia katika mapato ya halmashauri.”
Kufuatia maazimio hayo Frank Majingwa ambaye ni Mkulima Wilayani Busega, ameishukuru mamlaka hiyo kwa usimamizi na kusema awali hawakuwa na bei maalum ya kuuzia bidhaa zao lakini kwa sasa wataepukana na usumbufu uliokuwa ukijitokeza.
Licha ya makubaliano hayo, baadhi ya wanunuzi wa mazao ya Ufuta, Mbaazi, Dengu na Choroko akiwemo Mangua Mayele wameonesha kutoafiki wakisema utekelezaji wake utatoa taswira nzima ya namna biashara hiyo itakavyofanyika.