Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Isale unaolenga kunufaisha vijiji Sita vya Isale, Msilihofu, Ntuchi, Ifundwa, Kitosi na Nkata vilivyopo Wilayani Nkasi.
Ameyasema hayo leo Januari 30, 2025 Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maji, Injinia Andrew Kundo wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Bupe ambapo amesema Je lini Serikali itamaliza Mradi wa Maji Isale Wilayani Nkasi.
Amesema, “kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji (intake), ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 70.22, ujenzi wa matanki Sita (6) yenye jumla ya ujazo wa lita 420,000 na ujenzi wa vituo 75 vya kuchotea maji.”,
Kundo amesema, “utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 78 na umeanza kutoa huduma ya maji kwenye vijiji viwili vya Nkata na Kitosi.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2025 na kunufaisha wananchi 20,113 wa vijiji hivyo.”
Hata hivyo amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Kata za Kimnyak, Tarakwa, Kiranyi na Siwandeti Wilayani Arumeru.
“Kazi zinazofanyika katika mradi huo ni ujenzi wa tanki la kukusanyia maji. lenye ujazo wa lita 50,000, ununuzi na ufungaji wa pampu mbili zenye uwezo wa kuzalisha maji lita 1,560,000 kwa siku,”
“Ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa kilometa 67, pamoja na ujenzi wavituo 70 vya kuchotea maji, Utekelezaji wa mradi umefikia wastani wa asilimia 80 na umeanza kutoa huduma katika maeneo ya Olmringaringa na Kimnyaki kupitia vituo 13vilivyojengwa,” Amesema Kundo.
Amesema, Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2025 na utanufaisha wananchi wapatao 57,541 wa maeneo hayo.