Klabu ya Ken Gold haijataka kukata tamaa kama ilivyokuwa kwa Ihefu,Mbeya City wala Mbeya Kwanza. Timu hizo kwa sasa hazipo Ligi kuu ya NBC baada ya kushuka misimu michache iliyopita na sasa zinapambana kurejea tena Ligi kuu. KenGold mtazamo wao ni tofauti kabisa . Msimu huu wamecheza mechi 16 za ligi wakishinda mchezo 1 sare 3 na kufungwa mechi 12.
Kwa sasa wapo nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi na hawajakata tamaa kuamini huo ni mwisho wao . Ken Gold wana nafasi kubwa sana kusalia ligi kuu ikizingatiwa wana michezo 15 mbele yao yenye jumla ya alama 45 kama watashinda mechi zote.
Mipango ya KenGold
Mwanzoni mwa msimu KenGold ilikuja kwa staili ya kitofauti ikiwa imesheheni kikosi cha wachezaji wa kitanzania na waliotoka Championship. Kufanya vibaya ni kama kumewasanua matajiri wa klabu hiyo na kuamua kubadili gia angani kabla giza halijawa nene zaidi. Moja ya mambo waliyoyafanya ni usajili wa wachezaji wengi wazoefu wa ligi yetu,usajili wa mastaa kutoka nje ambao wamewahi kucheza ligi kuu ya NBC.
Mpango huu unakwenda kubadili taswira ya klabu na sasa inageuka kuwa tishio kwa wapinzani wake.Majina kama Emanuel Asante,Benard Morrison ,Miquisone ,Kelvin Yondani ni nembo ya Ken Gold kwa sasa. Naamini mipango yao kwa msimu huu itakuwa ni kusalia ligi kuu na msimu ujao kupambana kwa nguvu zote kama wanavyofanya Tabora United ambao msimu jana walicheza Play off na kuponea chupu chupu kushuka Daraja lakini leo hii wanaogopeka na kila kigogo na ni moja ya timu zinazopambana kumaliza nafasi nne za juu.
Ukanda wa Soka
Ukanda wa Mbeya ndio ukanda pekee wenye kutoa timu nyingi zinazoshiriki Ligi kuu kuanzia miaka ile ya Tukuyu Stars kikaja kizazi cha Tanzania Prisons ambao wanaubeba mkoa huo kwa sasa. Kizazi cha mpito kilichosheheni timu za Mbeya City,Ihefu na Mbeya kwanza na chenyewe kimekwenda likizo na sasa tupo kizazi cha Ken Gold . Mategemeo ya wanambeya yapo mikononi mwa Tanzania Prisons na Ken Gold wengi hawataki timu hiyo ipotee kwa sasa. sajili walizofanya zinakwenda kuwarudisha mashabiki hao uwanjani.
Februali Hii Ken Gold wanarudi vipi?
Ken Gold itaanza Raundi ya pili ya ligi ya NBC dhidi ya Yanga mchezo wa ugenini jijini Dar es salaam dimba la KMC Complex, Tarehe 10 watakuwa Mbeya kuwakaribisha Singida Black Stars kisha watasafiri kwenda Tabora tarehe 14 Februari kuwakabili Tabora United,Tarehe 18 Februari watawakaribisha Kagera Sugar jijini mbeya.Tarehe 22 Februari watawakaribisha KMC na Tarehe 24 FebruariĀ watavaana na JKT Tanzania dimba la Meja Generali Isamuyo kama watashinda mechi zote watakuwa na alama 18 jumlisha alama 7 walizonazo basi watakuwa na alama 25 sawa na Tabora United walio nafasi ya 5 kwa sasa