Serikali imesema inafanya jitihada Kituo cha Forodha cha Pamoja (OSBP) Kabanga, kinachotoa huduma kati ya Tanzania na Burundi, kiweze kutoa huduma saa 24  ili kiweze kuongeza ufanisi.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Ndaisaba George Ruhoho, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuwezesha Vituo vya Forodha vya Murusagamba na Kabanga, kufanya kazi saa 24.

Chande alisema kuwa Kituo cha Forodha cha Kabanga ni Kituo cha Pamoja (OSBP) cha kutoa huduma za forodha kati ya Tanzania na Burundi ambacho kina miundombinu wezeshi kama vile taa za ulinzi, vyombo vya ulinzi na usalama, na maeneo ya kukagulia bidhaa, wasafiri na wafanyakazi, hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi saa 24 kwa upande wa Tanzania.

“Ili Kituo hicho kiweze kutoa huduma saa 24, upande wa Kobero nchini Burundi unapaswa pia kuwa tayari kutoa huduma hizo saa 24”, alieleza Chande.

Alisema kuwa kwa sasa Kituo cha OSBP Kobero kwa upande wa Burundi kinatoa huduma kwa saa 12 tu, hivyo jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuwezesha mazingira ya Kituo cha OSBP Kobero kufanya kazi saa 24, hususan ulinzi na usalama.

Akieleza kuhusu Kituo cha Murusagamba, Chande alisema kuwa Kituo hicho ni kidogo cha forodha kinachofanya kazi ya uzuiaji (Preventive office), ambapo hufanya kazi ya kuzuia magendo kwenye maeneo ambayo mwenendo wa bidhaa na watu ni mdogo.

Tetesi za usajili Duniani Januari 31,2025
Wapewa mafunzo utekelezaji mkataba huduma kwa mteja