Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vitendea kazi ambapo sasa inatekeleza mradi wa ununuzi vifaa mbalimbali vya kuzima moto na uokoaji pamoja na magari 150 ya kuzima moto na uokoaji.
Bashungwa ameeleza hayo hii leo Februari 3, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai aliyetaka kujua Je, lini Serikali itanunua gari la Zimamoto Wilaya ya Ngorongoro.
“Kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa ununuzi vifaa mbalimbali vya kuzima moto na uokoaji pamoja na magari 150 ya kuzima moto na uokoaji” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa, pindi magari 150 ya kuzima moto na uokoaji yatakapofika nchini, yatasambazwa nchi nzima ikiwemo Wilaya ya Ngorongoro.
Aidha, amesema Serikali imewezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kununua magari 12 ya kisasa ambapo moja wapo lilitumiaka kuzima moto katika jengo gorofa la TRA Kariakoo.
Bashungwa amesema pia Serikali ipo mbioni kununua helikopta moja maalum kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambayo yataenda sambamba na kuwapatia Mafunzo Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Jeshi hilo.