Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Mahakama inatakiwa kuwa mwezeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutenda haki kwa usawa na kwa wakati.

Dkt. Samia ameyasema hayo hii leo Februari 3, 2025 wakati akiwahutubia, Majaji, wageni waalikwa pamoja na wananchi  kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, ambayo Kitaifa yamefanyika Jijini Dodoma.

Amesema, “Mahakama inatakiwa kuwa mwezeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa kutenda haki kwa usawa na kwa wakati. Kauli mbiu hii, (Tanzania ya 2050, nafasi za taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya maendeleo), inanipa faraja kwamba agizo langu nililolitoa wakati napokea taarifa ya kamati ya kuangalia taasisi ya haki jinai sasa linakwenda kufanyiwa kazi.”

Awali akiongea mahala hapo, Rais wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniface Mwabukusi amesema kuboresha maslahi na mazingira ya Mawakili na Mahakimu itakuwa ni kuwasaidia zaidi Wananchi.

“Kwakweli majengo yanavutia, teknolojia ni nzuri, lakini ni vema tuhakikishe tunaboresha maslahi na mazingira yao, kwa sababu ni hatari sana mwananchi mwenye shida kukutana na wakili mwenye stress ya kipato na hakimu mwenye stress ya kipato, hapa anayeshughulikiwa ni mwananchi, kwahiyo kuboresha maisha yao itakuwa ni kuwasaidia zaidi wananchi,” alisema Wakili Mwabukusi.

Watumishi BRELA wahimizwa uadilifu, nidhamu katika kazi
Azma ya Serikali ni kuhakikisha Wananchi wanapata Umeme wa uhakika - Kapinga