Swaum Katambo – Katavi.
Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mkoani Katavi kimelalamikia malipo kiduchu wanayoyapata pindi wanapokabidhiwa majalada kwa ajili ya kuendesha kesi za watuhumiwa wa makosa ya jinai ambapo wamedai kuwa malipo hayo hayawiani na uzito wa kazi.
Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mawakili Mkoa wa Katavi, Wakili Nassoro Ntenga katika kilele cha siku ya Sheria ambapo katika Mkoa wa Katavi yamefanyika katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi na kudai kuwa kiwango cha malipo wanachopewa ni kidogo.
“Mawakili wanapokuwa wamekabidhiwa jalada wamekuwa wakipokea wastani wa shilingi laki moja hadi laki tatu, ambapo ulipaji wa malipo hayo hutegemea tathmini inayofanywa na jaji husika kwa kadiri anavyoona inafaa”
“Mara nyingi mashauri haya huendeshwa kwa siku tatu mfululizo hadi wiki mbili, kiwango hiki cha malipo ni kidogo mnoo na mara nyingi kiwango hiki huwa hakikidhi gharama za usafiri kwenda Mahakamani. Pia licha ya udogo wa malipo kumekuwa na ucheleweshwaji wa malipo hayo kwa miezi mingi,” amesema.
Aidha chama hicho kimelalamikia uwepo wa utitiri wa Mawakili feki ‘Vishoka’ wanaofanya shughuli za Uwakili hali inayopelekea Mawakili halisi kukutana na nyaraka zisizo na vigezo na kupelekea kuharibu mashauri ya watu Mahakamani pamoja na kuchafua taswira ya Uwakili.
“Tunaiomba Serikali kushughulikia suala hili kwa haraka ili kulinda heshima ya tasnia yetu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kutoka kwa mawakili wenye weledi waliopewa jukumu hilo kwa mujibu wa Sheria,” ameongeza.
Akizunguza kwa niaba ya mgeni maalum Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf amesema anatambua kazi kubwa inayofanywa na Mahakama katika utatuzi wa migogoro ya wananchi hata hivyo amedai kuwa bado kuna changamoto katika migogoro ya ardhi.
“Tanzania ya 2050 ni ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya mifumo ya kidijitali ni vyema wadau wote wa haki madai tukaandaa na kuanza kuweka mifumo itakayoendana na Tanzania ya miaka 25 ijayo..,anzeni kuweka sawa mifumo yenu iendane na Tanzania tunayoitaka ya mwaka 2050 katika kutatua migogoro ya wananchi,” amesema.
Kwa upande wake mgeni rasmi Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi Gway Sumaye amesema katika maadhimisho hayo wameona jinsi ambavyo wananchi wameupenda na kuupokea mfumo wa kidijitali wa njia ya mtandao ambao husikiza na kutolea maamuzi kwa njia ya mtandao.
“Mfumo huu ni mfumo unaoleta tija kwa sababu ni mfumo unaotoa muda mfupi wa kesi kukaa mahakamani, mfumo huu ni wa kidijitali ambao kila mtu anao uwezo wa kuleta kesi yake popote na kusikilizwa akiwa hukohuko na baadaye maamuzi ya mahakama yanatolewa bila yeye kuja mahakamani.”
Maadhimisho ya ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu 2025 yamesindikizwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya 2050:Nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya Taifa ya maendeleo” huku Kitaifa yakifanyika katika makao makuu ya Nchi Dodoma na mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.