Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuinua na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kupitia vyombo vya Habari vya Kitaifa kama vile Redio, Televisheni, Makala za Magazeti na mitandao ya kijamii.
Ameyasema hayo Naibu waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la Mbunge Vitimaalum, Asha Abdullah ambapo aliuliza Serikali ina mpango gani wa kuinua lugha ya Kiswahili kupitia vyombo vyake vya Habari vya Kitaifa.
Anesema, “Serikali imeweka msisitizo kwa vyombo vya habari vya kitaifa, kuandaa na kurusha vipindi vinavyoelimisha, kuburudisha na kuhamasisha matumizi ya Kiswahili fasaha.”
“Vipindi hivi vinahusisha mijadala yakitaaluma, tamthilia, mashairi, na makala zinazochambua masuala ya lugha na utamaduni na Kwa sasa idadi ya vipindi imeongezeka hadi kufikia 35 kwa wiki,” amesema Mwinjuma.
Hata hivyo, amesema Serikali inajitahidi kushawishi watafiti kufanya tafiti kwa lugha ya kiswahili na kutafsiri tafiti ambazo walishazifanya kwa lugha nyingine iwe kwa lugha ya Kiswahili.
“ kwa kufahamu hilo baraza la kitaifa la Zanzibar wameandaa na kusanifu msamiati na utafiti wa Sayansi na teknolojia kwa lugha ya kiswahili, na machapisho kadhaa yameshachapishwa kwa lugha hiyo”,amesema
“Yakiwemo machapisho ya kamusi ya awali ya Sayansi na Teknolojia, lakini kamusi ya Fizikia, kemia na baiolojia na kamusi ya kompyuta na machapisho mengine kadha wa kadha,” amesema Mwinjuma.