Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa kwake na Kituo cha Huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kusema huduma duni zinasababisha malalamiko kutoka kwa wateja.
Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati wa Kikao cha Tatu cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2024 ikiwa ni utaratibu aliouanzisha kwa lengo la wa kujipima katika kila baada ya miezi mitatu ili kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara na Taasisi zake.
“Pamoja na kazi zote nzuri mnazozifanya lakini eneo ambalo bado hatujafanya vizuri ni utoaji wa huduma kwa wateja, juzi nilitembelea kituo hiki nikawaambia sifurahishwi na utendaji kazi wa kituo, mimi nafahamu changamoto za kituo hiki si kwa kuota bali wananchi wananipa mrejesho pamoja na viongozi wanaonisimamia,”
“Hivi tumefanya kazi yote hii ya kuwa na umeme wa ziada, tunajenga laini za umeme, lakini mtu mmoja ambaye kazi yake ni kumsikiliza mteja na kumpa majibu sahihi anatupaint wote vibaya tunaonekana hatufai, majibu yapo lakini wataalam wanageuka kuwa wababe kwa wateja, hii hakubaliki,” amesema Dkt. Biteko.
Ametolea mfano lalamiko la mwananchi la kupiga simu TANESCO kisha akapewa tiketi namba ya lalamiko lakini baada ya muda tiketi namba hiyo ilifutwa kwa madai kwamba lalamiko husika limeshashughulikiwa huku ikiwa sikweli, hata hivyo baada ya mteja kuuliza kwa nini lalamiko lake limefutwa aliishia kufokewa.
Kutokana na hilo, Dkt.Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuchukua hatua kwa mtaalam aliyehusika na suala hilo na endapo TANESCO haitachukua hatua ifikapo ijumaa wiki hii, atachukua hatua huku akisisitiza kwamba heshima kwa wananchi lazima iwepo na Wataalam wa Kituo cha Huduma kwa wateja wanapaswa kuwapa majibu stahiki na ya staha wananchi na wawe ni sehemu ya kutatua shida za wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameziagiza Taasisi zote chini ya Wizara ya Nishati kuupa kipaumbele Mpango wa Mahsusi wa Nishati (Energy Compact) ambao ulisainiwa katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Januari 28, 20225 ambao pamoja na masuala mengine ya nishati, umelenga kusambaza umeme kwa watanzania milioni 8.3 ifikapo 2030.