Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi ameiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kupitia baraza lake la wafanyakazi kuwasisitiza watumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na nidhamu ya kazi kutokana na watumishi wengi kwasasa kukiuka maadili ya utumishi wa umma.
Katibu Mkuu Maswi ameyasema hayo leo Februari 5,2025 Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa 23 wa baraza la wafanyakazi wa THBUB Mkoani Dodoma linalofanyika kwa siku mbili.
“Kama taasisi inayozingatia uzingatiaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, watumishi wa tume lazima muwe mfano bora utakao igwa na watumishi wengine wa umma tukija kwenu tunataka muwe mfano lakini pia msiwe na wasiwasi kuhusu utendaji wa tume,”amesema.
Amesema wao kuwa katika kikao cha baraza hicho ni kutokana na imani kubwa waliyopewa na wanzao hivyo watakaporudi waitishe mikutanao na viongozi wa kila idara ili wawaeleze yale waliyokubaliana na utelezaji wake.
“Mimi napenda kila mtu ajue kile mlichokubaliana hapa kwasababu kila idara ina mwakilishi wake,”amesema.
Pia, amesisitiza kuwa mikutano ya baraza la wafanyakazi itumike kujadili malengo, mipango ya taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi hivyo wanapaswa kuambizana ukweli juu ya yale yanayowasibu.
Awali Katibu Mtendaji wa THBUB na Mwenyekiti wa baraza hilo Patience Ntwina amesema lengo la mkutano huo ni kupitia taarifa za utekelezaji wa kazi za tume kwa mwaka 2023/2024 na 2024/2025 na kujadili mapendekezo ya mpango wa na bajeti ya mwaka 2025/2026.
“Pia tutajadili taarifa kuhusu hoja za wafanyakazi kwa ujumla na kwasababu wajumbe wa menejimenti wako hapa watapata wasaa wa kujibu kulingana na hoja zitakazojitokeza,”amesema.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa THBUB Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi (TUGHE) tawi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Pontian Kitorobombo amempongeza Katibu mkuu kwa kuwafungulia mkutano huo huku akiahidi kuwa watautumia kuhakikisha mwanapata haki yao na yakle yanayowasibu yanapatiwa majawabu.