Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amewaomba Watanzania kuendelea kuuenzi na kuudumisha Muungano kwani umeleta manufaa makubwa.

Amesema hayo wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa mwaka 2024 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Februari 05, 2025 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Joseph Mhagama.

“Muungano wetu ndio utaifa wetu tuendelee kuenzi Muungano wetu kwa maslahi mapana ya vizazi vijavyo na vinavyokuja. Muungano huu ni wa kipekee ukilinganisha na nchi zingine duniani zilizoungana lakini Muungano wao haukudumu,” alisema.

Khamis amesema, “hatuna budi kuwashukuru na kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwani kwa busara zao wamefanya kazi kubwa ya kuusimamia na kuulinda ambapo hivi Aprili 26, 2025 unatarajia kutimiza miaka 61 tangu kuasisiwa kwake.”

Ameongeza kuwa, uwepo wa Kamati ya pamoja imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha linapotokea jambo la mgongano, kamati hiyo inakutana kwa kwa pande zote mbili kwa lengo la kuhakikisha inatatua na Muungano unaendelea kuwa salama.

Amesema viongozi hao wakuu kupitia Serikali zote mbili wamefanya kazi kubwa na kuwazesha kupatiwa ufumbuzi wa changamoto za Muungano zaidi ya 15 na kuufanya uendelee kudumu.

Kuhusu hoja ya uwepo wa Ofisi za Muungano kwa upande wa Zanzibar, Khamis amefafanua kuwa zipo Taasisi 33 zinazohusa Muungano na tayari 21 zina majengo ambayo yana ofisi zake.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Mhagama amesema Bunge limeazimia Serikali ihakikishe ihakikishe ujenzi wa ofisi na majengo ya kudumu kwa upande wa Zanzibar ili kurahisisha utoaji wa wahuduma kwa wananchi.

Hivyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepokea na kukubali taarifa ya shughuli za Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria Miundombinu kwa mwaka 2024 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Februari 5, 2025.

Masauni azindua Mradi wa utunzaji vyanzo vya Maji
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Februari 6, 2025