Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Upendo Naftali ameongoza kikao cha kupanga mikakati ya usambazaji wa mbegu za Alizeti aina ya Sunbloom, ambapo Halmashauri hiyo imepokea jumla ya tani 12 za mbegu kutoka kwa Wakala wa Mbegu za Serikali (ASA), wakilenga kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaongezeka.
Akiongoza Kikao hicho, kilichohudhuriwa na Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo, Maafisa Elimu Kata, pamoja na Watendaji Kata mjini Singida, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa kata na maafisa ugani ili kufanikisha malengo ya kuongeza uzalishaji wa alizeti.
Amesema, lengo kuu la kikao hicho ni kuhakikisha kuwa mbegu za alizeti zinawafikia wakulima katika kata zote 18 za manispaa, ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima wa alizeti, huku akieleza kuwa usambazaji wa mbegu hizo unafanyika kwa haraka ili kutoa fursa kwa wakulima kupanda mbegu hizi kwa wakati na kuvuna mavuno bora.
“Kikao hiki kimejikita katika kuhakikisha kwamba usambazaji wa mbegu unakuwa na mpangilio mzuri ili kuepuka changamoto zozote zinazoweza kuzuia wakulima kufaidika na fursa hii muhimu ya kilimo cha alizeti,” alisema Upendo.
Wakulima wa alizeti katika manispaa ya Singida wanatarajiwa kupata mbegu bora zitakazowawezesha kuongeza tija katika kilimo cha Alizeti na hivyo kuchangia katika maendeleo ya Kilimo cha mazao ya Biashara ikiwemo kukuza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla.