Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Soko la Bidhaa Tanzania, TAMISEMI, Sekta Binafsi, Taasisi za Fedha, Mamlaka ya Biashara Tanzania na wadau wengine wa maendeleo imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha mfumo wa Stakabadhi za Ghala Nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Febuari 7 Jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo hatua hizo zinaendelea kuchukuliwa ikiwa ni siku ya kuhitimisha msimu wa biashara ya bidhaa za kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa mwaka 2024/2025.
Amesema, wanapojiandaa na kuanza msimu mpya wa biashara wa 2025/26, ni vyema kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana, changamoto tulizokabiliana nazo, na mikakati ya kuimarisha mfumo huu kwa msimu ujao.
“Katika msimu wa 2024/2025, jumla ya bidhaa 14 zilikusanywa na kuuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, zikiwemo Chai, Choroko, Dengu, Kahawa, Kakao, Korosho, Maharage, Mahindi, Mbaazi, Mchele, Mihogo, Mpunga, Soya, na Ufuta.”
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, tulishuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji na ukusanyaji wa mazao, ambapo jumla ya kilogramu 810,230,588 zilikusanywa, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 80% ikilinganishwa na msimu wa 2023/2024, ambapo kilogramu 451,192,592 zilikusanywa”. Amesema Jafo
Amesema Ongezeko hili halikuakisiwa tu katika kiwango cha mazao bali pia katika thamani ya mapato ya wakulima.
“Kutokana na wingi wa bidhaa pamoja na kuimarika kwa bei sokoni, wakulima walilipwa jumla ya Shilingi Trilioni 2.9, ongezeko la 142% ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 1.2 walizopata msimu uliotangulia, hali hii ni uthibitisho wa jinsi Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unavyoendelea kuwa chombo madhubuti cha kuhakikisha wakulima wananufaika ipasavyo na jasho lao”
“Pamoja na faida kwa wakulima, ongezeko hili la thamani limezinufaisha pia halmashauri zilizoshiriki katika Mfumo huu, na mapato yatokanayo na ushuru yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 36 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia Shilingi Bilioni 87 msimu huu wa pili
unaokamilika”. Amesema Jafo
Hata hivyo amesema hiyo ni ishara wazi kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala siyo tu unawanufaisha wakulima bali pia unachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali za Mitaa, na hivyo kusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.