Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameeleza kuwa Miji yote 12 ya kundi la kwanza walioanza utekelezaji wa miradi ya barabara na mifereji ya maji ya mvua kwa kusaini mikataba kwa pamoja tarehe 23 Septemba, 2023 na wakandarasi kuanza utekelezaji tarehe 20 Novemba, 2023 kwa mikataba ya miezi 15, miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 19 Februari, 2025.

Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa fupi ya Mradi wa Uboreshaji Miundombnu ya Miji (TACTIC) Awamu ya II unaotekelezwa chini ya TARURA katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa soko kuu la Majengo pamoja na ujenzi wa Kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni jijini Dodoma.

Mhandisi Seff amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza katika mkoa wa Dodoma ni ujenzi wa barabara kiwango cha lami Km 10.21, mtaro wa maji ya mvua Ilazo Km 2.1, uboreshaji wa mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua (3), mitaro ya kutiririsha maji Km 2.81 pamoja na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu wa miradi.

Ameeleza kuwa barabara zinazojengwa ni barabara ya Mbuyuni SP2 Km 1.69, Mauma-Makutano mita 760, Mbuyuni-Mwangaza Km 2.56 na Ntyuka-Mkalama-Mapinduzi Km 5.2 ambapo mkandarasi ni M/s China Geo-Engineering Corporation ambapo thamani ya mkataba ni shilingi bil. 24.1 na muda wa utekelezaji ni miezi 15.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika miji 12 ya kundi la kwanza ni ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala, masoko ya bidhaa na mazao mbalimbali, bustani za mapumziko na vivuko maji.

Amesema katika jiji la Dodoma kazi za ujenzi zitakazofanyika ni uboreshaji wa soko kuu la majengo na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, uboreshaji stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, ujenzi stendi ya mabasi madogo Nzuguni na ujenzi wa vivuko maji katika maeneo ya Chaduru, Mailimbili na Ntyuka.

Amebainisha kuwa mkandarasi atakayetekeleza mradi ni M/s Azhar Construction Company Limited kwa mkataba wenye thamani ya shilingi bil. 14.2 na muda wa utekelezaji ni miezi 12.

Tuwajibike kulinda usalama wa Raia na Wanadiplomasia - Ruto
Picha: Rais Samia ashiriki mkutano wa Wakuu wa SADC, EAC