Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), William Ruto amesema Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, unaheshimu mipaka na uhuru wa kila taifa, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha usalama wa raia, wanadiplomasia na walinda amani.

Ruto ameyasema hayo hii leo Februari 8, 2025 katika Mkutano wa Pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC, Ikulu jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa kutojali maisha ya watu na kushambulia balozi na walinda amani ni kinyume na sheria za Kimataifa.

Amesema, “kama wanachama wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaheshimu mipaka na uhuru wa kila taifa. Tunawajibika kuhakikisha usalama wa raia, wanadiplomasia, na walinda amani katika nchi zetu. Kutojali maisha ya watu na kushambulia balozi na walinda amani ni kinyume na sheria za kimataifa na ni kitendo cha kikatili.”

Aidha, Ruto amesema anatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa DRC kusitisha mapigano mara moja na kushiriki katika mazungumzo yenye lengo la kurejesha amani.

“Hasa, tunatoa wito kwa kundi la M23 kusitisha mashambulizi yao na kwa jeshi la DRC kuepuka hatua za kulipiza kisasi. Kusitisha mapigano mara moja kutatoa nafasi ya mazungumzo ya kujenga na utekelezaji wa makubaliano ya amani ya kudumu,” alisisitiza Ruto.

ARV zipo za kutosha, puuzeni taarifa za uzushi - Wizara
Mradi wa TACTICS kwa miji 12 kukamilika Februari