Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,  Ridhiwani Kikwete amelieza Bunge mikakati mitano inayofanywa na Serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa Vijana nchini na namna kumudu ushindani kwenye soko la ajira.

Ridhiwani ameyasema hayo hii leo Februari 10, 2025 bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpendae (CCM), Toufiq Turky aliyehoji kuna mpango gani wa kuwandaa vyema vijana waweze kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya Tanzania ili kukabiliana na upungufu wa ajira nchini.

Ameitaja mipango hiyo ya Serikali akisema ni kuwaandaa vijana ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Ridhiwani amesema, mipango hiyo ni pamoja na kubuni na kutekeleza programu maalum zinazowawezesha vijana kujifunza kwa vitendo kupitia sekta zinazozalisha ajira kwa wingi kama vile sekta ya kilimo kupitia programu ya Jenga Kesho iliyobora (BBT), ujasiriamali, na madini kupitia Programu ya Mining for a better Tommorrow (MBT).

Pia, amesema kufanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Tolea la Mwaka 2023 ambayo yanasisitiza mafunzo kwa kuandaa wataalamu.

“Kupitia ujenzi wa miundombinu ya Kimkakati muhimu inayochochea uchumi, vijana wameajiriwa na kunufaika na urithishwaji ujuzi kutoka kwa wataalamu wa nje mfano ujenzi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na barabara za mwendokasi (BRT),” amesema Mhe. Kikwete

Kadhalika, amesema Serikali itaendelea kubuni na kutekeleza programu ya kukuza ujuzi ambayo inalenga kukuza ujuzi kwa nguvu kazi ili kuwezesha vijana kushindana katika soko la ajira mfano mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo kazini na kwa wajasiriamali.

Waziri Ridhiwani amesema mkakati mwingine ni kuweka msisitizo kwenye matumizi ya TEHAMA katika kuzalisha fursa nyingi za ajira kwa vijana.

“Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha vijana wanaandaliwa ili wapate ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na hivyo kumudu ushindani wa ajira,” amesema.

Mtandao wa Malonjo wavunjwa Dodoma, mmoja adakwa na Mirungi
Mita za Maji za malipo kabla kusambazwa Manyara