Kibaha, Pwani – Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amekabidhi hundi ya mfano ya Shilingi milioni 917 kwa vikundi 76 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani iliyopo Mlandizi, ikihudhuriwa na wanufaika wa mkopo pamoja na Wananchi.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwakamo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo, akisema hatua hiyo itawasaidia wananchi kuepuka mikopo yenye masharti magumu. Amehimiza wanufaika kurejesha fedha hizo kwa wakati ili wengine pia wapate fursa ya kunufaika.
Amesema, “kuna dhana potofu kwamba fedha hizi ni ruzuku au sadaka. Naagiza vikundi vyote kurejesha mikopo kwa wakati ili mfuko huu uwe endelevu.”
Aidha, amewakumbusha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuanzia Februari 13 hadi 19, 2024, akibainisha kuwa zoezi hilo linawahusu waliotimiza miaka 18, waliohama makazi, na waliopoteza vitambulisho vyao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Shukuru Lusanjala amesema Halmashauri imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo hiyo, ambapo katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya Shilingi 917,329,000 zimelenga vikundi 76, wakiwemo wanawake (Shilingi 466,452,000), vijana (Shilingi 409,371,000), na watu wenye ulemavu (Shilingi 41,500,000).
Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya vikundi kushindwa kurejesha mikopo yao kama inavyotakiwa, huku Kaimu Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amepongeza usimamizi mzuri wa mikopo hiyo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, akisema chama kinaridhishwa na utendaji wake.