Uwepo wa Kituo cha Mfano cha Katente katika Mkoa wa Kimadini Mbogwe umeleta mapinduzi katika ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali kufuatia Wachimbaji Wadogo wa Madini kukitumia kituo hicho kuchenjua mawe yao jambo ambalo limewezesha ukusanyaji wa kodi mbalimbali na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa madini ya dhahabu.
Hayo yamebainishwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe Mhandisi Jeremiah Hango wakati akizungumza na Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini Ofisini kwake Februari 10, 2025, waliotaka kufahamu manufaa ya uwepo wa kituo hicho kwenye shughuli za uchimbaji mdogo.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Mkoa huo wa kimadini umeshuhudia mafanikio kutokana na kusogeza huduma kwa wachimbaji ikiwemo kituo hicho na hivyo kupelekea mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji mdogo kuongezeka ambapo katika Mwaka wa Fedha 2021/22 mkoa huo ulikusanya shilingi bilioni 21.3, Mwaka wa Fedha 2022/23 shilingi bilioni 22.4 na Mwaka wa Fedha 2023/24 kiasi cha bilioni 27.1 kilikusanywa.
‘’Tangu kuanza mwaka huu wa fedha tayari tumekwishakusanya shilingi bilioni 18 na kwa mwenendo huu tunaamini tutavuka malengo ya makusanyo tuliyoweza kukusanya katika kipindi kilichopita”, amesema Mhandisi Hango na kuongeza kwamba, mwaka huu wa fedha mkoa huo umepangiwa kukusanya shilingi bilioni 45.
Aliongeza kuwa, Mkoa wa Kimadini Mbogwe ulioanzishwa mwaka 2021, ukisimamia wilaya tatu ikiwemo Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale kwa lengo la kusogeza huduma kwa wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake mafanikio makubwa yameshuhudiwa.
Pia, alisema, uwepo wa Kituo cha Mfano Katente ni muhimu kwa Mkoa wa Kimadini Mbogwe ambapo wachimbaji wanapata huduma bora na za uhakika pamoja na kupata ushauri wa namna bora ya utunzaji wa mazingira.
“Naomba nitumie fursa hii kuwataarifu wadau wote wa Sekta ya Madini kukitambua na kukitumia Kituo chetu cha Mfano Katente kina wataalamu wa kutosha na wenye maadili hivyo niwahamasishe wachimbaji wote wa Mbogwe kupeleka material yenu katika kituo hicho kwa ajili ya uchenjuaji salama na wenye tija”, alisema Mhandisi Hango.
Akizungumzia changamoto ya mahitaji makubwa ya uchenjuaji kituoni hapo, alisema kutokana na mahitaji ya wachimbaji, Serikali ina mpango wa kuongeza ukubwa wa kituo hicho ili kukidhi mahitaji ya wachimbaji.
Pamoja na mambo mengine, alitoa wito kwa wananchi na wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani humo ikiwemo ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji (CIP), uuzaji wa vifaa vya uchimbaji, uchimbaji wenyewe, biashara ya madini pamoja na shughuli mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa shughuli hizo.
Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo, alisema tayari Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na tayari Serikali imetoa leseni za uchimbaji zaidi ya 300 na kuna baadhi ya maeneo mchakato wa upatikanaji wa leseni unaendelea na kueleza kwamba, Serikali inaendelea kuthamini wachimbaji wadogo mkoani humo.
Vituo vya Mfano vilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora na wa kisasa wa madini usio athiri mazingira naunaohamasisha matumizi ya teknolojia rahisi katika shughuliza uchimbaji mdogo. Hadi sasa kuna jumla ya vituovitatu vya mfano vilivyoko katika maeneo ya Lwamgasa-Geita, Katente-Bukombe na Itumbi-Chunya.