Idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa Ugonjwa wa UKIMWI, huenda yakaongezeka mara sita zaidi Duniani ifikapo mwaka 2029 ikiwa Marekani itashikilia msimamo wake wa kukata mpango kukabiliana na ugonjwa huo.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na Ugonjwa wa Ukimwi, Winnie Byanyima ambaye amesema mamilioni ya watu wanaweza kufa na aina mpya sugu ya virusi hivyo inaweza kuibuka.

Byanyima, amesema maambukizi ya virusi vya Ukimwi yamekuwa yakipungua katika miaka ya hivi karibuni, huku visa vipya milioni 1.3 pekee vikirekodiwa kwa mwaka 2023, likiwa ni punguzo la asilimia 60 tangu maambukizi hayo yalipokithiri mnamo mwaka 1995.
“Tangu tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba nchi yake itakatiza misaada yote ya kigeni ndani ya siku 90, maafisa wanakadiria kuwa ifikapo mwaka 2029, huenda kukawa na maambukizi mapya milioni 8.7 ya virusi vya Ukimwi, vifo milioni 6.3 vinavyohusishwa na ugonjwa huo pamoja na mayatima milioni 3.4,” alifafanua Byanyima.