Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeweka mwongozo wa gharama za kuunganisha umeme kwa wateja, ambapo gharama hizo hutofautiana kulingana na hali ya eneo.
Kapinga ameyasema hayo leo Februari 11, 2025 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu aliyeuliza Serikali inatofautishaje Kaya maskini Vijijini na Mijini katika kuwaunganishia umeme nchini.
“Kulingana na mwongozo huo, maeneo yanayotambuliwa kama miji na vijiji miji, gharama ya kuunganisha umeme ni shilingi 320,960 na kwa maeneo ya vijiji gharama ya kuunganisha umeme ni shilingi 27,000,” amesema Kapinga.
Kapinga ameongeza kuwa miradi ya umeme inatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha kwa makundi tofauti tofauti na kusisitiza kuwa miradi ambayo wateja wanalipia shilingi 27,000, ni kwa ajili ya Vijijini na ni miradi ambayo Serikali inaweka ruzuku, ili wananchi wapate umeme kwa gharama nafuu.
Amesema, kwa maeneo ya miji na Vijiji miji ipo miradi mingine ijulikanayo kama Peri-urban, ambayo inawaunganisha wananchi wa maeneo hayo kwa shilingi 27,000 na kuongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuunganisha kipindi miradi hiyo inatekelezwa.