Waandikishaji daftari la kudumu la wapiga kura Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wametakiwa kizingatia kanuni na taratibu walizoelekezwa ili kukamilisha shughuli hiyo kwa ufanisi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmahauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani Dkt. Rogers Shemwelekwa wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa maafisa hao 262 yaliyofanyika Mjini humo.
Amesema, “hii kazi ni ya kitaifa hivyo muende mkaitekeleleze kwa kuzingatia maelekezo mliyopewa wakati wa mafunzo.”
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/b4f84b73-1b18-4a18-af84-e2058dea5e0e.jpg)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani, Dkt. Rogers Shemwelekwa akifunga mafunzo kwa waandikishaji wa daftari la kudumu lawapiga kura yaliyifanyika kwa siku mbili Mjini humo.
Shemwelekwa amesema kuwa ni vema maafisa hao wakatambua kuwa kazi wanayoenda kuifanya ni ya kizalendo na si ya kujipatia maslahi makubwa hivyo suala la uaminifu wanapaswa kuliweka mbele zaidi.
“Msijiwekee matumaini ya kupata pesa za vikoba kupitia kazi hii bali mtambue kwamba mnaenda kufanyakazi ya uzalendo malipo mnayolipwa ni ya kawaida,” amesema.
Baadhi ya wakazi Mkoa wa Pwani wamesema kuwa suala la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lina umuhimu mkubwa hivyo ni vema waandikishaji hao wakazingatia weledi katika utoaji wa huduma hiyo.
“Waandikishaji wazingatie kanuni kama walivyoelekezwa ikiwemo ratiba na kutoingiza upendeleo kwa ndugu jamaa na marafiki zao hasa kuwapa kipaumbele hata kama wamechelewa kufika” amesema Meshak John.
Kwa upande wake Neema Saimon amewataka wakazi wa mji huo kutumia muda vizuri wa kujiandikisha na si kusubiri siku ya mwisho kwani kutawaweka kwenye wakati mgumu.
“Wengi wamezoea kusubiri siku za mwishoni ndipo wanajitokeza kwenda kujiandikisha sasa hiyo ni hatari na inaleta shida ni bora ukaenda kujiandikisha siku za mwanzoni inakupa uhuru na nafasi ya kwenda kufanya majukumu mengine,” amesema.
Shughuli ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Halmashauri ya Mji wa Kibaha itafanyika kwa siku saba kuanzia Februari 13 – 19, 2025 huku vituo 131, vikitarajia kutumika.