Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewakaribisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
Akizungumza jijini New Delhi nchini India katika Mkutano wa Mawaziri wa Nishati kutoka India, Sudan, Malawi, Rwanda, Nepal, Brazili pamoja na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kutoka India Dkt. Biteko amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha kuwa Nishati Safi ya Kupikia inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.
Ambapo mwaka 2022 Serikali ilisisitiza matumizi ya nishati safi na kueleza athari za matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwa kuanzisha mjadala wa kwanza ambao uliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akitaja fursa mbalimbali za biashara ya Nishati Safi ya Kupikia nchini Tanzania, kama vile ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji, kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia.
Fursa zingine ni vituo vya kupokea LPG, vifaa vya uhifadhi, miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na maeneo jirani, usambazaji wa LNG wa kiwango kidogo, vifaa na mitungi ya gesi asilia.
“ Hivyo basi, ningependa kuchukua fursa hii kuwataka wadau wote na wawekezaji katika sekta ya nishati kujiunga nasi katika malengo yetu makubwa lakini yanayoweza kufikiwa ya kupata umeme na nishati safi ya kupikia safi, kuongeza sehemu ya nishati mbadala katika mchanganyiko wa nishati na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi ili kusaidia upatikaji wa nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Hata hivyo, ametaja jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia akisema, “Tanzania imekamilisha maendeleo ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa mwaka 2024-2034 wenye lengo kuu la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.”

Magari ya Serikali mbioni kutumia Gesi asilia
Serikali yawataka Wanasheria wa Halmashauri kuzingatia weledi