Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado ina fursa nyingi za Uwekezaji katika Sekta mbalimbali na kuwakaribisha Wawekezaji kutoka Saudi Arabia kuwekeza nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Saudi Arabia waliofika Ikulu kuonana naye wakiwa katika ziara maalum Tanzania ya kubaini maeneo ya Ushirikiano na Uwekezaji pamoja na Biashara.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/476983227_941725908136392_3947621558404175092_n.jpg)
Aidha Rais Dkt.Mwinyi amezitaja sekta nyengine ambazo zina fursa za Uwekezaji ni Kilimo, Mafuta na Gesi na Miundombinu na kuushukuru Ujumbe huo kwa kuamua kuja Zanzibar kwani Ziara hiyo itafungua ukurasa mpya wa Ushirikiano wa baina ya nchi hizo mbili na kuwasisitiza kuwa Mabalozi wazuri wa kuzitangaza fursa ziliopo nchini kwao.
Naye Rais wa Shirikisho la Jumuiya za Wafanyabiashara wa Saudi Arabia Hassan Alhuwayz amesema wana nia ya dhati ya kuimarisha Ushirikiano na Zanzibar hususani katika masuala ya Biashara na Uwekezaji kwani tayari wamebaini kuwepo kwa fursa nyingi pamoja na kuvutiwa na Maendeleo yaliyofikiwa na Zanzibar na hali ya Amani iliopo.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/479956284_941725854803064_2529662264836081515_n.jpg)
Wakati huo huo Rais Dkt.Mwinyi alishuhudia Utiaji wa Saini wa Mikataba baina ya Zanzibar na Saudi Arabia ikiwemo Mkataba wa Ushauri kati ya Zanzibar na Kampuni ya Saudi Arabia African Investment and Development Company na Mkataba wa Ushirikiano baina ya Jumuiya ya kitaifa ya Wafanyabiashara wa Zanzibar (ZNCC).
Mkataba mwingine uliotiwa saini ni ule wa Shirikisho la vyama vya Wafanyabiashara wa Saudi Arabia kwa lengo la kuimarisha Uwekezaji wa kimkakati na kukuza Uchumi wa Zanzibar.