Watu wawili, John Peter (45), Dereva na Mkazi wa Manyire Wilayani Arumeru Mkoani Arusha na Jafari Shirima (62) Dereva na Mkazi wa Singida, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kusababisha ajali iliyopelekea kifo cha mtu mmoja Lucy John (40), mkazi wa Manyire.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo imeeleza kuwa tukio hilo lililotokea Februari 12, 2025 majira ya saa 08:00 usiku huko Nganana barabara ya Afrika Mashariki ambapo Mtuhumiwa John Peter aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 499 CRR aina ya Toyota Noah aligonga kwa nyuma gari lilokuwa limeegeshwa barabarani.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/11111.jpg)
Gari hilo lililogongwa kwa nyuma ni Lori lenye namba za usajili T 629 CLB aina ya Scania likiwa na tela lenye namba za usajili T 447 BSL likiendeshwa na Dereva Jafari Shirima ambapo tukio hilo lilisababisha kifo cha Lucy John ambaye alikuwa abiria katika gari aina ya Toyata Noah.
Taarifa ya Kamanda Masejo imeeleza kuwa mara baada ya kugonga gari hilo kwa nyuma mtuhumiwa John Peter alimshambulia Dereva wa Lori Jafari Shirima na kitu chenye ncha kali na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo anaendelea kupatiwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi.