Mafunzo ya kuwajengea uwezo Watoa Huduma za Afya juu ya uboreshaji wa Mawasiliano kati ya Mtoa huduma na Mteja (Interpersonal Communication-IPC) yana mchango mkubwa katika kuleta Ufanisi Huduma za Chanjo.
Hayo yamebainishwa Wilayani Babati Mkoani Manyara na Mganga mkuu wa Wilaya ya Hanang, Dkt. Ally Mohammed Kodi wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo hayo katika Mkoa wa Manyara ambayo yanafanyika katika Halmashauri mbili za Babati na Hanang yakiratibiwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/11.png)
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hanang Dkt. Ally Mohammed.
“Kama tunavyofahamu chanjo ni muhimu sana kwa watoto na watu wazima na inasaidia kuzuia magonjwa yayozuilika kwa njia ya chanjo kama vile Surua, na Polio kwa hiyo Watumishi wakipata Mafunzo haya uboreshaji wa Mawasiliano kati ya Mtoa Huduma na Mteja utaleta ufanisi wa huduma za chanjo kwani itachochea wananchi kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma,” amesema.
Lotalis Gadau ni Afisa Programu wa Mafunzo, Uhamasishaji, na Uelimishaji Jamii kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo amesema huduma za utoaji wa chanjo kwenye jamii ziko vizuri ambapo kiwango cha utoaji wa chanjo kwa mwaka jana ilikuwa zaidi ya asilimia 95% ambapo pia mafunzo hayo yataongeza zaidi uimarishaji wa mawasiliano kwa baadhi ya maeneo kati ya Mtoa huduma na Mteja.
![](https://dar24.com/wp-content/uploads/2025/02/22.png)
Afisa Programu wa Mafunzo, Uhamasishaji, na Uelimishaji Jamii kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo, Lotalis Gadau.
“Mwaka jana kiwango cha huduma ya utoaji wa chanjo ilikuwa 95% hivyo kiwango kiko vizuri tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan , hivyo na matarajio yetu baada ya mafunzo haya ni kuimarisha zaidi mawasiliano baina ya Mtoa Huduma na Mteja na mtoto anapokamilisha ratiba za chanjo tunategemea milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo haitakuwepo ”amesema.
Kwa upande wake Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma amezungumzia umuhimu wa elimu ya afya kuhusu matumizi sahihi ya chanjo kwa lugha inayoeleweka katika jamii.
Amesema, “unaweza ukawa na huduma nzuri na hiyo isipate wateja, na chanjo ni huduma nzuri sana kwa jamii hivyo ili wananchi waielewe vizuri na mafunzo haya ya kuwajengea uwezo watoa huduma na tunaendelea kuwasisitiza kuwa wateja wanapokuja katika vituo vya huduma za afya isiishie tu kumchoma sindano ya chanjo au matone ya chanjo lazima pia mteja apewe elimu umuhimu wa chanjo katika Kinga ya Mwili.”
Beatrice Kiluwa pamoja na Lucas Kwilasa ni baadhi ya Watoa Huduma za Afya walionufaika na Mafunzo hayo wamesema kupitia Mafunzo hayo itarahisisha kujenga mahusiano mazuri na wateja na kuimarisha ubora wa huduma katika vituo vya Kazi.