Waandishi wa Habari wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wanawake kuhusu umuhimu wa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Tunguu.
Amesema, licha ya Waandishi kufanya kazi kubwa ya kuelezea changamoto zinazowakumbaWanawake kwenye kuwania nafasi za uongozi na kueleza umuhimu wa kuwa na uwiano sawa katika nafasi za uongozi, bado kuna kazi ya kuwaelimisha, ili waongeze ujasiri wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.
“Wanawake wengi wana uwezo wa kuongoza, lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa kujiamini. Hili ni jambo ambalo waandishi wa habari wanapaswa kulifanyia kazi kwa kuandaa vipindi vinavyoelimisha na kuwahamasisha wanawake,” aliongeza Dkt. Mzuri.
Aidha, amesema Redio zimekuwa zikiifanya kazi kubwa katika kutangaza mambo yanayohusu jamii, hivyo waandishi wanapaswa kuendelea kuandaa vipindi vyenye tija vinavyohamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Kuhusu kaulimbiu ya Siku ya Redio Duniani kwa mwaka huu isemayo “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi” Dkt. Mzuri amesema vyombo vya habari vinatakiwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na namna ya kupambana na ongezeko la joto duniani.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria maadhimisho hayo, wamesema Redio nyingi kwa sasa zimejikita katika masuala ya kibiashara, badala ya kutoa maudhui yanayolenga maendeleo ya jamii na baadhi ya vipindi vimekuwa sehemu za ushabiki, hasa kwenye michezo, ambapo mijadala mingi inajikita kwenye timu za Simba na Yanga badala ya kuzungumzia changamoto za kijamii.
Aidha, wamependekeza Redio kurejea katika misingi ya awali kwa kutoa maudhui yanayolenga maendeleo ya jamii, hasa katika kuwawezesha Wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi, wakikumbuka kwamba wana jukumu kubwa la kuwaelimisha na kuwahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.
Ikumbukwe kwamba kupitia Redio, Wanawake wanaweza kupata taarifa sahihi na motisha ya kushiriki katika siasa, hatimaye kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla, huku jamii nayo ikipata habari ambazo zinalenga uhalisia wa maisha ya Mwanadamu na mambo yanayomzunguka ili kujiletea maendeleo.