Mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Delcat Idengo amefariki kwa kupigwa risasi wakati alipokuwa akirekodi video ya muziki wake mpya huko mji wa Goma uliopo Kivu Kaskazini.
Msanii huyo, anayejulikana kwa nyimbo zake zenye kuikosoa Serikali, alikuwa ametoka kuachia wimbo wake mpya mtandaoni unaowalaani Wapiganaji wa M23 na ADF kama vikosi vya uvamizi huko Goma.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema, Idengo ambaye alikuwa amevalia mavazi ya kijeshi kwa ajili ya upigaji picha wa video, alishambuliwa karibu na eneo la Kilijiwe na alikufa papo hapo baada ya risasi kumpiga kichwani.
Mwimbaji huyo alikuwa mmoja wa wafungwa 4,400 waliotoroka gereza la Munzenze lililopo Goma, wakati mji huo ulipotekwa na wapiganaji wa M23 baada ya mapigano mafupi mwezi Januari na amefariki katika tukio hilo la Februari 13, 2024.