Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amesema ameridhishwa na kasi inayoendelea katika kilimo cha zao la pamba huku akiwasisitiza wataalamu kuendelea kuwafikia wakulima katika maeneo yao na kuwaelimisha matumizi ya vifaa vya kisasa ikiwemo ndege ndogo zisizokuwa na rubani (drone) katika kuboresha zao hili ambapo zinatumika kunyunyizia dawa shambani, ndege ambazo zimepelekwa na Bodi ya Pamba.
Hayo ameyasema wakati akifanya ukaguzi, hamasa na ufuatiliaji wa kilimo cha zao la pamba wilayani Kishapu ambapo pamoja na mambo mengine RC Macha amesema kuwa uwepo wa vifaa hivyo vya kisasa unamuwezesha mkulima kunyunyizia dawa katika shamba lenye ukubwa wa Hekari moja kwa dakika sita pekee, jambo ambalo linatajwa kuwa mkombozi mkubwa wa mkulima wa zao la pamba mkoani Shinyanga.
“Nimefuatilia na kukagua mashamba yenu ndugu zangu niseme kuwa nimeridhishwa sana na kasi ya kilimo cha zao hili la pamba hapa wilayani Kishapu, hakika sasa tunakwenda kurejesha heshima ya zao la pamba kama ilivyokuwa hapo awali na hili ndiyo kusudio la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kilimo hiki cha pamba kinakuwa ni chenye tija zaidi kwenu na kuchechemua uchumi wa wananchi pamoja na kuongeza pato la Taifa,” amesema RC Macha.
RC Macha akiwa ameongozana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson na wataalamu wengine ambapo amesisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuona kila mkulima wa zao la pamba anahakikisha kuwa kila Hekari moja (1) inazalisha kuanzia Kilo 1000 hadi 1200.
Hiki ni kiwango ambacho kinatajwa kuwahi kufikiwa hapo awali ambapo walikuwa wanafikia hadi Kilo 1800 kwa Hekari moja na hivyo kukifanya kilimo cha zao la pamba kuwa ni moja kati mazao ya biashara na yenye tija zaidi kwa wananchi na muktadha mzima wa ustawi wa jamii kwa ujumla.
Huu ni mwendelezo wa ziara za RC Macha za kuwafikia wakulima moja kwa moja huko walipo, katika maeneo yao ikiwemo mashambani akiwa na lengo la kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unarejea katika hadhi na ramani yake ya awali katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, elimu, uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuwa na nishati ya umeme wa uhakika, maji na huduma zote muhimu katika vijiji vyote 506 hapa mkoani Shinyanga.