Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imesaini Hati za Makubaliano (MoU) na Kampuni za GF Truck, Apollo Heavy Equipments, na META kwa lengo kurahisisha upatikanaji wa mitambo ya kisasa kwa wachimbaji wadogo nchini.
Hayo yameelezwa leo Februari 14, 2025 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu aliyetaka kujua ni lini Serikali itawapatia leseni, mitambo na mitaji wachimbaji wadogo wa Singida Mashariki.
Katika majibu yake, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo ya uchimbaji kupitia maombi ya mtu mmoja mmoja yanayowasilishwa kwa Tume ya Madini. Aidha, Serikali imetenga maeneo maalum kwa wachimbaji wadogo katika Mkoa wa Singida, yakiwemo Mhintiri, Londoni, na Sambaru.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, STAMICO kupitia vituo vya mfano inaendelea kutoa huduma ya ukodishaji wa vifaa muhimu kama vile compressors na pampu za maji kwa gharama nafuu ili kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini.
Amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini nchini, ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni, upatikanaji wa mitambo, na uwezeshaji wa kifedha ili kuboresha shughuli za uchimbaji na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Aidha, ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao, Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, STAMICO imeingia makubaliano na taasisi za fedha kama CRDB, NMB, AZANIA, na KCB. Kupitia taasisi hizi, wachimbaji wadogo wanaweza kupata mikopo kwa masharti nafuu ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji.
Naibu Waziri Dkt. Kiruswa amebainisha kuwa, kwa lengo la kuwaelimisha Wachimbaji Wadogo kuhusu fursa hizo, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na STAMICO na Tume ya Madini imekuwa ikiendesha semina na makongamano katika mikoa mbalimbali nchini na kwamba Semina hizo zinawawezesha Wachimbaji Wadogo kuelewa taratibu za kupata maeneo, mitambo, na mikopo ili kuongeza ufanisi katika sekta ya madini.
Hatua hizo za Serikali zinadhihirisha dhamira yake ya kuhakikisha Wachimbaji Wadogo wanapata msaada unaohitajika ili kuboresha shughuli zao, kuongeza vipato vyao na kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi.